Wokovu


Wokovu kwa jumla unamaanisha kuondolewa hali isiyopendeza au ya hatari kabisa.

Kwa namna ya pekee, katika Ukristo Historia ya Wokovu ni wazo la msingi: maana yake ni kwamba, katika mfululizo wa matukio ya dunia hii, Mungu anawakomboa binadamu kutoka dhambi zao na kutoka matokeo yake katika maisha ya duniani na katika uzima wa milele.

Biblia ya Kikristo inatamka kuwa neema ya Mungu ndiyo inayookoa watu, kwa kuwa hao hawawezi kujikomboa peke yao, lakini wanapokea wokovu kama zawadi (neema, dezo) kwa njia ya imani.

"Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu" (Waraka kwa Waefeso 2:8).

Heusler Allegory of Salvation
Mfano wa Wokovu kadiri ya Antonius Heusler (1555), National Museum huko Warsaw, Poland.

Wokovu katika Agano la Kale

Katika Biblia neno "wokovu" linatafsiri maneno mbalimbali yanayohusu kuondolewa mabaya ya kimwili na ya kiroho vilevile. Daima Mungu ndiye asili yake. Ndiye anayeokoa kwenye vita (Kutoka 15:2), ajali (Zaburi 34:6), mikono ya adui (2 Samueli 3:10), uhamisho (Zaburi 106:47), kifo (Zaburi 6:4), dhambi (Ezekieli 36:29).

Kwanza Waisraeli walifikiria hasa wokovu wa kidunia kwa taifa lao, lakini polepole kwa kuzingatia uovu, walifikia hatua ya kuona wokovu upande wa maadili na kuhusu mataifa mengine pia (Isaya 49:5,6; 55:1-5).

Kadiri yao, wokovu unapatikana kwa njia ya uadilifu uliotazamwa kama utekelezaji kamili wa Torati.

Wokovu katika Agano Jipya

Maneno ya Kigiriki yanayotumiwa na Agano Jipya kumaanisha "kuokoa" na "wokovu" ni: σώζω (sōzō) e σωτηρία (sōtēria). Maana yake asili ni kuopoa kwa nguvu kutoka hatari (k.mf. ya ugonjwa).

Kwa kawaida Yesu alionyesha wokovu kuwa ni ukombozi kutoka dhambi ambao uanze kung'amuliwa mapema, ingawa utakamilika ahera: "Mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka" (Injili ya Mathayo 10:22; 24:13).

Hasa Mtume Paulo alisisitiza wokovu ni tunda la kifo na ufufuko wa Yesu Kristo, aliyeleta baraka zote kumpitia Roho Mtakatifu, kama vile wongofu, kuzaliwa upya, utakaso, kufanywa mwana, utakatifu na utukufu.

Ndiyo utatuzi wa tatizo la dhambi uliotolewa na Mungu.

Siku ya mwisho matokeo ya wokovu yatahusu ulimwengu wote ambao utajumlishwa pamoja na historia yote katika Kristo, aliye Alfa na Omega (Waraka kwa Warumi 8:21,22; Waefeso 1:10).

Wokovu katika teolojia ya Kikristo

Kutokana na mwelekeo wa watu wa magharibi, suala la masharti ya wokovu limeshika nafasi kubwa katika teolojia kuanzia Agostino wa Hippo, wakati masuala ya kinadharia zaidi yakitawala Ukristo wa mashariki.

Ni suala hilo lililosababisha Matengenezo ya kiprotestanti katika karne ya 16 na linaendelea kujadiliwa sana katika nchi zilipokea Ukristo kutoka nchi za magharibi.

Hata hivyo katika miaka ya mwisho, Wakatoliki, Walutheri, Wamethodisti, Wakalvini na Waanglikana wamefaulu kukubaliana kuhusu suala hilo.

Marejeo

  • Atkin, James. The Salvation Controversy. San Diego, Calif.: Catholic Answers, 2001. ISBN 1-888992-18-2
  • Jackson, Gregory Lee. Justification by Faith: Luther versus the U.O.J. [i.e. "Universal Objective Justification" Lutheran] Pietists. [Glendale, Ariz.]: Martin Chemnitz Press, 2012. ISBN 978-0-557-66008-7
  • Lutheran World Federation and Roman Catholic Church. Joint Declaration on the Doctrine of Justification. English language ed. Grand Rapids, Mich.: W. B. Eerdmans Publishing Co., 2000. ISBN 978-0-8028-4774-4

Viungo vya nje

Christianity Symbol.png Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wokovu kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Agano Jipya

Agano Jipya ni sehemu ya pili ya Biblia ya Kikristo, ikifuata Agano la Kale: Agano Jipya limefichika katika lile la Kale, na Agano la Kale limedhihirika katika lile Jipya.

Linakusanya vitabu ambavyo Wakristo wote wanaviheshimu kama vitakatifu na vilivyoandikwa baada ya ujio wa Yesu Kristo hadi mwisho wa wakati wa mitume wake.

Vitabu vyake 27 vinaleta habari zake, za mitume wake na za mwanzo wa Kanisa lake.

Vinatakiwa kusomwa kama kilele cha ufunuo wa Mungu kwa binadamu kadiri ya Historia ya Wokovu.

Jina lilitungwa na nabii Yeremia (Yer 31:30) alipotambua kwamba kwa kiasi fulani lile la mlima Sinai lilikuwa na dosari (Eb 8), lakini Mungu kwa uaminifu wake asingeweza kukubali likome tu.

Vitabu vya Agano Jipya ni kama ifuatavyo (Kwa mabano: kifupi cha kawaida kwa kutaja kitabu hiki).

Biblia ya Kikristo

Biblia ya Kikristo ni mkusanyo wa maandiko matakatifu ya Ukristo. Maandiko hayo mbalimbali yanaitwa tangu zamani sana "vitabu" tu, inavyomaanishwa na neno la Kigiriki βιβλια, "biblia" ambalo ni wingi wa neno "biblos" yaani "kitabu".

Hutofautishwa na Tanakh ambayo ndiyo maandiko matakatifu ya dini ya Uyahudi na ambayo pengine inatajwa kwa jina lilelile la "Biblia", hasa katika matoleo ya Biblia ya Kiebrania. Vitabu vyake vimo katika sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo kwa jina la "Agano la Kale".

Biblia ya Kikristo hugawiwa sehemu mbili ambayo ni Agano la Kale na Agano Jipya. Agano la Kale lina maandiko yaliyoandikwa kabla ya Yesu Kristo na vitabu vya Agano Jipya viliandikwa baada yake.

Dhambi

Dhambi ni kosa la kiumbe mwenye hiari dhidi ya uadilifu unaompasa.

Inaweza kufanyika kwa mawazo, maneno, matendo na kutotimiza wajibu.

Maadili yanamuelekeza binadamu katika kutambua dhambi ni zipi pamoja na madhara yake.

Kwa kawaida dini zinahusianisha kosa hilo na Mungu aliye asili ya uadilifu, kwa kuwa ndiye aliyeumba viumbe vyote na kuvielekeza maishani.

Akiwapa baadhi ya viumbehai akili na utashi, papo hapo Mungu amewapa wajibu wa kufuata maelekezo yaliyomo katika utaratibu wa nafsi yao na wa ulimwengu wote.

Katika dini zinazofundisha kwamba Mungu alitoa ufunuo wake hata kwa njia ipitayo maumbile, ni dhambi kwenda kinyume cha ufunuo huo, kwa mfano unavyopatikana katika vitabu vitakatifu vya dini husika, kama vile Biblia kwa Wayahudi na Wakristo na Kurani kwa Waislamu.

Kutokana na uenezi wa dhambi kuanzia dhambi ya asili, linajitokeza suala la wokovu, ambalo linaweza kutazamwa zaidi kama neema, lakini kwa kawaida linadai toba ya mkosefu.

Kanisa Katoliki na hata baadhi ya madhehebu mengine ya Ukristo linaamini linaweza kuondolea dhambi yoyote katika ubatizo na kitubio kwa kutumia mamlaka ambayo Yesu mfufuka aliwashirikisha Mitume wake alipowavuvia akisema: “Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yoh 20:22-23). “Mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu” (1Kor 6:11).

Ekumeni

Ekumeni ni tapo la Ukristo linalolenga kurudisha umoja kamili kati ya madhehebu yake mbalimbali.

Msingi wake ni imani inayowaunganisha katika Yesu Kristo na kwa njia yake katika Utatu mtakatifu, yaani Mungu pekee aliye Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Neno linatokana na Kigiriki oikouméne, linalomaanisha kwa asili sehemu ya dunia iliyokaliwa na watu; hivyo likaja kuwa na maana ya jambo linalohusu waamini duniani kote.

Ekumeni ilianza kati ya Waprotestanti, hasa lilipofanyika Kongamano la Kimisionari la Kimataifa huko Edimburg, mwaka 1910, ambapo waliohudhuria walisisitiza uhusiano kati ya umoja wa Wakristo na kazi ya uinjilishaji wa mataifa yote.

Mwaka 1937 iliundwa Halmashauri ya Kiekumeni ya Makanisa, ikijumlisha hata Waorthodoksi. Kwa sasa inawakilisha robo tu ya Wakristo wote, kwa sababu Wakatoliki na Wapentekoste wengi hawajajiunga na muundo huo.

Hata hivyo Kanisa Katoliki liliingia kwa nguvu katika juhudi za ekumeni kuanzia Papa Yohane XXIII (1958-1963) na Mtaguso wa pili wa Vatikano (1962-1965).

Historia ya Wokovu

Kwa jina hilo Wakristo wanamaanisha ufafanuzi wa mpango wa kazi ya Mungu kwa wokovu wa binadamu kadiri ya Biblia.

Imani

Imani kwa Kiswahili ni neno lenye maana mbalimbali (k.mf. "huruma"), lakini ile kuu inahusiana na kitenzi kuamini, kinachofanana na kusadiki. Hapo ni kukubali ukweli wa jambo lisiloweza kuthibitishwa.

Katika dini msingi wake ni mamlaka ya Mungu aliyeshirikishwa ukweli huo kwa njia ya ufunuo maalumu ili kumsaidia binadamu amjue yeye, ajifahamu pamoja na maisha yake duniani na ahera.

Kwa msingi huo, au wa namna hiyo, mtu anaweza kushikilia jambo bila ya uthibitisho mwingine, ingawa pengine Ukristo unatia maanani pia akili katika ujuzi wa ukweli.

Kadiri ya Mtume Paulo imani ikifuatana na tumaini na upendo ni adili kuu mojawapo, msingi, mzizi na chanzo cha wokovu.

Injili ya Luka

Injili ya Luka ni kitabu cha tatu katika orodha ya vitabu vya Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo. Huhesabiwa kati ya Injili Ndugu pamoja na Injili ya Mathayo na Injili ya Marko.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Kanisa Katoliki

Kanisa Katoliki ni jina linalotumika kwa maana mbalimbali, lakini hasa kumaanisha Kanisa la Kikristo linalokubali mamlaka ya kiroho ya Papa wa Roma kama mkuu wa urika wa maaskofu juu yake lote.

Ndilo kubwa kabisa kati ya madhehebu yote ya dini hiyo, likikusanya nusu ya wafuasi wote wa Yesu.

Hata hivyo, Wakristo wa madhehebu mengine wanaokubali kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli wanatafsiri tofauti sehemu yake inayokiri Kanisa la kweli kutambulishwa na sifa nne, ya tatu ikiwa kwamba ni katoliki: "Tunasadiki Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume".

Kanisa Katoliki, likiwa na miaka karibu elfu mbili, ni kati ya miundo ya zamani zaidi iliyopo duniani na imechangia kwa kiasi kikubwa ustaarabu wa Magharibi, ingawa tangu mwishoni mwa Karne za Kati athari yake inazidi kupungua, ilivyo wazi leo hasa katika masuala yanayohusu jinsia na uzazi.

Imani ya Kanisa hilo inatokana na ufunuo wa Mungu ulivyotolewa kwa Israeli na ulivyokamilishwa na Yesu ambaye alimtambulisha kama Baba na alilianzisha kwa njia ya Roho Mtakatifu aliyetumwa naye juu ya Mitume wake siku ya Pentekoste mwaka 30 (au 33) BK.

Ni imani inayoungamwa katika ubatizo, sakramenti ya kwanza na mlango wa sakramenti nyingine sita: kwamba Mungu ni mmoja tu katika nafsi tatu: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Imani hiyo inatakiwa kutekelezwa katika maadili maalumu yanayotegemea hasa upendo ambao ndio adili kuu na uhai wa mengine yote.

Kutokana na juhudi za kutekeleza matendo ya huruma kwa yeyote mwenye shida, Kanisa Katoliki linatoa huduma za elimu na afya kuliko taasisi nyingine yoyote duniani kote.

Kama vielelezo vya utakatifu ambao waamini wote wanaitiwa, Kanisa linapendekeza watu wa Agano la Kale na wa Agano Jipya, hasa Bikira Maria, lakini pia wale waliojitokeza zaidi katika historia yake kama watakatifu.

Baadhi yao wana wafuasi wengi wanaounda familia za kiroho, mara nyingi kama mashirika ya kitawa yenye karama mbalimbali.

Kanisa la Kilatini

Kanisa la Kilatini (wakati mwingine "Kanisa la Kiroma") ni moja ya madhehebu yanayounda Kanisa Katoliki. Ndiyo kubwa kuliko yote (97% za waumini wote), likiwa na Wakristo zaidi ya bilioni 1 duniani kote.

Mengine ni Makanisa Katoliki ya Mashariki (3%) yanayofuata mapokeo na hasa liturujia kama ya Waorthodoksi lakini yakiwa na ushirika kamili na Papa wa Roma ambaye ndiye mkuu wa Kanisa la Kilatini, pamoja na kwamba ni pia mkuu wa Kanisa Katoliki lote.

Jina linatokana na kwamba kwa karne nyingi lugha pekee iliyotumika katika ibada zake ilikuwa Kilatini.

Kanisa hilo lote upande wa sheria linafuata Mkusanyo wa sheria za Kanisa, kumbe upande wa liturujia wengi wa waamini wake wanafuata mapokeo ya Kanisa la Roma, lakini wengine wanafuata mapokeo ya Ambrosi wa Milano, au yale ya Lyon, Braga, Toledo na ya mashirika mbalimbali ya kitawa (k.mf. Wakartusi na Wadominiko).

Hivi karibuni waamini waliotokea madhehebu ya Anglikana wameruhusiwa kuendelea kutumia baadhi ya matini yake katika ibada wakiwa sasa ndani ya Kanisa la Kilatini.

Liturgia

Liturgia (pia: liturujia na liturugia; kutoka Kigiriki λειτουργια, leiturgia, yaani huduma kwa umati wa watu) ni utaratibu wa ibada hasa katika Kanisa la Kikristo.

Wakati mwingine neno hili linatumika pia kwa muundo au utaratibu wa sala katika dini mbalimbali.

Kwa kawaida liturgia inamaanisha utaratibu maalumu unaoweka mpangilio wa sala, nyimbo, masomo na sherehe nyingine wakati wa ibada.

Taratibu zinatofautiana kulingana na imani, teolojia, historia na utamaduni wa wahusika.

Hivyo ndani ya Ukristo kuna taratibu mbalimbali ambazo matawi yake makuu ni:

liturgia ya Waorthodoksi na Waorthodoksi wa Mashariki

liturgia ya Wakatoliki wanaofuata mapokeo ya Roma

liturgia ya madhehebu ya Uprotestanti wa asili (Walutheri, Waanglikana, Waprebiteri n.k.), tofauti na ubunifu wa yale ya Wapentekoste n.k.Kiini cha liturgia ya Kikristo ni zile ibada zilizoanzishwa na Yesu mwenyewe, hasa ekaristi.

Liturujia ya Braga

Liturujia ya Braga ni liturujia maalumu inayotumika tangu karne ya 6 hasa katika jimbo kuu la Braga (Ureno).

Inahusiana na aina nyingine za liturujia ya Kilatini, kama vile liturujia ya Toledo na liturujia ya Roma.

Baada ya Mtaguso wa pili wa Vatikano, jimbo kuu la Braga limeamua (1971) mapadri waweze kuendelea kwa hiari yao na liturujia hiyo au kutumia ile ya Roma.

Liturujia ya Kilatini

Liturujia ya Kilatini ni aina ya liturujia ya Ukristo iliyoenea upande wa magharibi wa Dola la Roma ambapo ilitumika lugha ya Kilatini.

Liturujia hiyo ilistawi Ulaya magharibi na Afrika kaskazini.

Polepole liturujia ya Roma, mji mkuu wa Walatini uliotawala dola hilo, ilienea katika maeneo mengi ya Kanisa Katoliki, hasa kutokana na juhudi za makusudi za kaisari Karolo Mkuu za kuunganisha mataifa yaliyokuwa chini ya himaya yake.

Baadaye Mtaguso wa Trento ulizidi kudai Wakatoliki wa magharibi wafuate wote liturujia ya Roma, isipokuwa kama liturujia yao maalumu yaliendelea zaidi ya miaka 200.

Hivyo baadhi ya liturujia nyingine za Kilatini zimedumu mpaka leo, kama vile liturujia ya Ambrosi kandokando ya Milano (Italia), liturujia ya Kimozarabu hasa huko Toledo (Hispania), liturujia ya Braga huko Ureno na kidogo liturujia ya Lyon huko Ufaransa.

Pia baadhi ya mashirika ya kitawa yanatunza liturujia za pekee.

Liturujia ya Lyon

Liturujia ya Lyon (kwa Kilatini: ritus Lugdunensis) ni liturujia mojawapo ya Kanisa la Kilatini ambayo imeendelea kutumika katika jimbo kuu la Lyon (Ufaransa) tangu karne ya 9 hadi leo, ingawa kwa kuzidi kufifia, hasa baada ya Mtaguso wa pili wa Vatikano.

Msalaba wa Yesu

Msalaba wa Yesu ni msalaba ule ambao Yesu Kristo alisulubiwa juu yake huko Yerusalemu kwa amri ya Ponsyo Pilato siku ya Ijumaa, labda tarehe 7 Aprili 30 BK.

Tukio hilo, pamoja na ufufuko wa Yesu unaosadikiwa na Ukristo kutokea siku ya tatu (Jumapili ya Pasaka), ndiyo kiini cha imani ya dini hiyo mpya iliyotokana na ile ya Uyahudi.

Kwa Wakristo fumbo hilo la Pasaka ndilo kilele cha historia ya wokovu inayotangazwa na Biblia ya Kikristo.

Fumbo hilo lilisababisha kazi nyingi za sanaa ya Kikristo, hasa uchoraji na uchongaji.

Mtakatifu

Mtakatifu ni binadamu aliye hai au aliyekufa ambaye dini fulani au watu mbalimbali wanamheshimu kwa namna ya pekee kwa jinsi alivyoonekana kuwa karibu zaidi na Mungu hata akashirikishwa utakatifu wake. Kwa hiyo hutazamwa kama kielelezo cha uadilifu na pengine kama mwombezi pia.

Mungu Baba

Mungu Baba ni nafsi ya kwanza ya Mungu katika imani ya Wakristo (isipokuwa Wasiosadiki Utatu).

Sifa nne za Kanisa

Sifa nne za Kanisa, kadiri ya imani ya madhehebu mengi ya Ukristo, ni zile ambazo zinalitambulisha Kanisa la kweli kati ya makundi mengi ya Ukristo ni kuwa moja, takatifu, Katoliki, la Mitume.

Sifa hizo zilitajwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) uliporefusha Kanuni ya Imani iliyotungwa na Mtaguso wa kwanza wa Nisea (325).

Ndiyo sababu zinakubaliwa na madhehebu mengi, ingawa zinatafsiriwa nayo kwa namna tofautitofauti.

Uprotestanti

Uprotestanti ni aina ya Ukristo iliyotokana na Kanisa Katoliki huko Ulaya Kaskazini katika karne XVI kufuatana na tapo la kidini na la kisiasa maarufu kwa jina la "Matengenezo ya Kiprotestanti". Wahusika wakuu wa tapo hilo ni Martin Luther na Yohane Kalvini.

Urika wa maaskofu

Urika wa maaskofu ni msamiati wa teolojia ambao unatokeza imani ya Kanisa katika umoja wa sakramenti ya daraja takatifu katika ngazi yake ya juu kuhusu utekelezaji wa kazi tatu ambazo Yesu aliwaachia Mitume wake na waandamizi wao kwa njia yao.

Maaskofu wote wanaunda kundi hilo kutokana na sakramenti waliyopokea, hata wasipoongoza jimbo lolote.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.