Uario

Uario (au Uariani) ni msimamo wa teolojia ambao unamuita Yesu "Mwana wa Mungu" lakini kwa kukanusha imani ya Wakristo karibu wote kuhusu Utatu mtakatifu, yaani uwemo wa nafsi tatu za milele katika Mungu pekee: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Hivyo unafafanua kwamba Yesu Kristo si sawa na Mungu Baba wala si wa milele, bali ni kiumbe tu, ingawa bora kuliko wote.[1]

Jina linatokana na lile la Ario (250 hivi – 336), padri wa Aleksandria, Misri. Ingawa yeye hakuwa wa kwanza kufafanua hivyo maneno ya Yoh 14:28, mafundisho yake yalivuruga kabisa Kanisa kwa muda mrefu na kuhitaji mitaguso mikuu miwili ili kuyakomesha katika Dola la Roma.[2][3]

Kwa ajili hiyo, katika mitaguso hiyo ya kiekumeni ya kwanza (Mtaguso wa kwanza wa Nisea na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli) ilitungwa ikapanuliwa kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli iliyotakiwa kufuatwa na maaskofu wote, hata kwa nguvu ya serikali ya Dola la Roma.

Juhudi hizo hazikuzuia Uario kuendelea nje ya dola hilo, hasa kati ya makabila ya Kijerumani ambayo muda mfupi baadaye wakavamia Dola la Roma na kudhulumu Wakatoliki, hasa Hispania na Afrika Kaskazini.

Mwanzoni mwa karne za kati, Uario uliachwa kabisa, lakini ukatokea tena na tena, hasa nchini Marekani.

Hivyo Uario unafuatwa hata leo na madhehebu kadhaa ya Ukristo, ambayo kwa sababu hiyo yanatazamwa na wengine wote kama si Wakristo ama walau ni Wakristo wa pembeni (kwa Kiingereza "Marginal Christians"). Mfano wake ni Mashahidi wa Yehova, Wamormoni, lakini pia baadhi ya Wapentekoste.

Baptism of Christ - Arian Baptistry - Ravenna 2016
Mozaiki ya paa la Ubatizio wa Kiario.

Tanbihi

  1. Williams, Rowan (2002). Arius: heresy and tradition. Wm. B. Eerdmans Publishing Co, 98. ISBN 978-0-8028-4969-4.
  2. Socrates of Constantinople, Church History, book 1, chapter 33. Anthony F. Beavers, Chronology of the Arian Controversy.
  3. First Council of Constantinople, Canon 1. ccel.org.
Christianity Symbol.png Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uario kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Aleksanda wa Aleksandria

Aleksanda I wa Aleksandria (alifariki tarehe 26 Februari au 17 Aprili, 326 au 328) alikuwa Patriarki wa 19 wa Aleksandria, Misri. Wakati wa uongozi wake alikabili masuala mbalimbali, kama vile tarehe ya Pasaka, matendo ya Meletius wa Lycopolis, na hasa Uario. Ndiye aliyekuwa mpinzani mkuu wa padri Ario na wa mafundisho yake hadi Mtaguso wa kwanza wa Nisea. Ndiye aliyemuandaa shemasi Atanasi wa Aleksandria kuwa mwandamizi wake.Tangu kale anaheshimiwa na Waorthodoksi wa Mashariki, Waorthodoksi na Wakatoliki kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 26 Februari au 29 Mei.

Apolinari wa Laodikea

Apolinari wa Laodikea (alifariki mwaka 390) alikuwa mwanateolojia aliyefundisha kwamba Yesu hakuwa na akili ya kibinadamu; badala yake alisema Yesu Kristo alikuwa na mwili na upande wa chini tu wa roho (zinapotokea hisia) lakini akili yake ilikuwa ya Kimungu.

Inaonekana alifundisha hivyo katika juhudi za kupinga Uario uliokanusha umungu wa Yesu.Baada ya kupingwa na Theodoreto wa Kuro na Basili Mkuu, fundisho hilo lililaaniwa na Sinodi ya Aleksandria ya mwaka 362, iliyoongozwa na Atanasi wa Aleksandria, na hatimaye kutajwa kama uzushi na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381), uliosisitiza kwamba Kristo ni Mungu kamili na mtu kamili.

Ario

Ario (kwa Kiberberi: Aryus ; kwa Kigiriki Ἄρειος, Areios, 250 au 256 – 336) alikuwa padri kutoka Libya aliyefanya kazi huko Alexandria, Misri.Mafundisho yake yalisisitiza kuwa Mungu Baba ni mkuu kuliko Mwana, akipinga imani katika Utatu.Kristolojia yake ilikanushwa na askofu wake, Aleksanda wa Aleksandria, lakini ilienea kote mashariki mwa Dola la Roma na kuvuruga Kanisa Katoliki kiasi cha kudai Kaisari Konstantino I aitishe Mtaguso wa kwanza wa Nisea mwaka 325.

Huo mtaguso mkuu wa kwanza, uliokusanya maaskofu wengi hasa wa mashariki, ulikataa hoja zake na kumkiri Mwana kuwa na hali ileile ya Baba.

Hata hivyo vurugu ziliendelea hata kudai ufanyike mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (383), ambao ni wa pili kati ya mitaguso ya kiekumene, nao ukasisitiza na kukamilisha imani ya mtaguso wa kwanza wa Nisea katika Kanuni ya Imani ya Nisea-Konstantinopoli.

Ingawa imani hiyo ilikubaliwa kura rasmi katika Dola la Roma, Uario ulienea kati ya makabila ya Kijerumani, hasa Wagoti na Wavandali, hivyo uliendelea hadi karne ya 7 na ya 8.

Mpaka leo kuna madhehebu yanayokanusha umungu wa Yesu Kristo na kusema ni kiumbe tu.

Efrem wa Syria

Efrem wa Siria (kwa Kiaramu: ܐܦܪܝܡ ܣܘܪܝܝܐ, Aphrêm Sûryāyâ; kwa Kiarabu أفرام السرياني; kwa Kigiriki: Ἐφραίμ ὁ Σῦρος, Ephraim Syros; kwa Kilatini: Ephraem Syrus) (Nisibi, leo nchini Uturuki, 306 hivi - Edesa, leo nchini Uturuki, 9 Juni 373), alikuwa mtawa na shemasi, mwanateolojia na mwanashairi pamoja.

Ni maarufu hasa kwa tenzi zake nyingi ajabu kwa lugha ya Kiaramu ambazo zinatumika hadi leo katika liturujia na kutokeza imani kwa namna bora.

Ndiye mwakilishi muhimu zaidi wa Ukristo wa Kisiria.

Kisha kufa akaheshimiwa na Waorthodoksi wa Mashariki, Waorthodoksi na Wakatoliki kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Papa Benedikto XV tarehe 5 Oktoba 1920 alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 9 Juni, siku ya kifo chake kilichotokea Edesa mwaka 373.

Eugenius wa Karthago

Eugenius wa Karthago (alifariki 13 Julai 505) alikuwa Mkristo aliyechaguliwa kwa kauli moja kuwa askofu wa Karthago mwaka 480 baada ya Deogratias wa Karthago (aliyefariki 456).

Ilimbidi apambane na Uario ulioungwa mkono na mfalme wa Wavandali ili kutetea imani sahihi. Alifaulu kuwavuta baadhi yao katika Kanisa Katoliki na kwa sababu hiyo alifukuzwa akaishi uhamishoni katika jangwa la Libia.

Baadaye aliruhusiwa kurudi, lakini miaka minane baadaye akafukuzwa tena ahamie Vienne, karibu na Albi (Ufaransa). Huko alijenga monasteri aliposhika maisha ya toba hadi kifo chake.

Fulgensyo wa Ruspe

Fulgensyo wa Ruspe (Fabius Claudius Gordianus Fulgentius; Thelepte, leo Medinet-el-Kedima, 462 au 467 – Ruspe, 1 Januari 527 au 533) alikuwa mmonaki, mwanateolojia na askofu wa Ruspe (leo nchini Tunisia)

Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake.

Hati ya Thesalonike

Hati ya Thesalonike (maarufu pia kwa jina la Cunctos populos) ilitolewa tarehe 27 Februari 380 BK. Iliagiza raia wote wa Dola la Roma kukiri imani ya maaskofu wa Roma na Aleksandria, ikifanya Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya dola hilo.

Leandri wa Sevilia

Leandri wa Sevilia (Cartagena, leo nchini Hispania, 534 hivi - Sevilia, Hispania, 13 Machi 600 au 601) alikuwa askofu mkuu wa Sevilia ambaye alifaulu kuingiza katika Kanisa Katoliki kutoka Uario Wavisigoti waliotawala Hispania na Ureno wa leo, kuanzia Hermengildi na Rekaredo, watoto wa mfalme.

Tangu zamani anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Machi au 27 Februari.

Paulo I wa Konstantinopoli

Paulo I wa Konstantinopoli (mzaliwa wa Thesalonike (Ugiriki), alifariki mwaka 350 hivi), alikuwa askofu wa sita wa Konstantinopoli kuanzia mwaka 337. Paulo alijihusisha na mabishano kuhusu Uario yaliyoshughulikiwa na ndugu Makaisari Constans (Dola la Roma Magharibi) na Constantius II (Dola la Roma Mashariki).

Basi Paulo alitawazwa na kuondolewa mara tatu kati ya miaka 337 na 351.

Hatimaye aliuawa akiwa uhamishoni huko Cucusus, mkoani Kapadokia (leo nchini Uturuki).

Anaheshimiwa tangu kale kama mtakatifu mfiadini.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 7 Juni au tarehe 6 Novemba.

Petro wa Sebaste

Petro wa Sebaste (340 hivi – 26 Machi 391) alikuwa askofu wa mji huo, Sebaste katika Armenia Ndogo.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu, sawa na kaka zake Basili Mkuu, Gregori wa Nisa, na dada yao Makrina Mdogo, ambao walimuathiri sana tangu utotoni.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 26 Machi.

Remigius wa Reims

Remigius au Remi wa Reims, (kwa Kifaransa: Rémi au Rémy; Cerny-en-Laonnois, karibu na Laon, Picardy, 437 – Reims, Champagne, 13 Januari 533) alikuwa askofu wa Reims (Ufaransa) anaheshimiwa kama mtume wa Wafaranki. Tarehe 25 Desemba 496 alimbatiza mfalme Clovis I na kwa njia hiyo alivutia Wafaranki wengi katika Ukristo, jambo muhimu sana katika historia ya Kanisa na ya Ulaya kwa kuwa hilo lilikuwa kabila la kwanza la Wagermanik kuingia Kanisa Katoliki bila kupitia Uario halafu lilitawala sehemu kubwa ya Ulaya magharibi na kuunda ustaarabu wake.

Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki, Waorthodoksi na Waanglikana kama mtakatifuOctober 1 (translation of relics).

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe ya kifo chake.

Serapioni wa Thmuis

Serapioni wa Thmuis (300 hivi - Thmuis, 370 hivi), alikuwa askofu wa mji wa Thmuis (leo Tell el-Timai) nchini Misri na mwandishi wa Kikristo kwa lugha ya Kigiriki.

Tangu kale anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa. Sikukuu yake inaadhimishwa na Wakatoliki tarehe 21 Machi au 7 Machi.

Theodosius Mkuu

Flavius Theodosius (11 Januari, 347 – 17 Januari, 395) alikuwa Kaizari wa Dola la Roma kuanzia 15 Mei, 392 hadi kifo chake.

Kabla hajatawala dola zima, alikuwa Kaizari upande wa Mashariki kuanzia Agosti 378. Upande wa Mashariki alimfuata Valens.

Theodosius alikuwa Kaizari wa mwisho aliyetawala dola zima la Roma. Ndiye aliyetangaza Ukristo wa Kikatoliki kuwa dini rasmi ya dola.

Hati ya Thesalonike ilisisitiza imani moja tu kuwa halali katika dola la Roma, ile "katholiki" (yaani, isiyo ya sehemu) na "orthodoksi" (yaani, sahihi).

Tangu hapo, Theodosius alitumia nguvu nyingi kuzima aina zote za Ukristo tofauti na hiyo, hasa Uario.Hati hiyo ilifuatwa mwaka 381 na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli, uliothibitisha na kuongezea ungamo la Nisea katika Kanuni ya imani ya Nisea-Konstantinopoli.Mwaka 383, Kaisari alidai madhehebu mengine yote yampatie maungamo yao ya imani, akayachambua na kuyachoma yote isipokuwa ya Wanovasyani. Hivyo madhehebu hayo hayakuruhusiwa tena kukutana, kuweka mapadri wala kueneza mafundisho yao. Theodosius alikataza wazushi wasiishi tena Konstantinopoli, na miaka 392-394 alitaifisha maabadi yao.Baada yake wanae wawili walishiriki utawala, Honorius upande wa Magharibi, na Arcadius upande wa Mashariki.

Waorthodoksi wanamheshimu kama mtakatifu. Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 17 Januari.

Uapolinari

Uapolinari ni fundisho la Apolinari wa Laodikea (alifariki mwaka 390) kwamba Yesu hakuwa na akili ya kibinadamu; badala yake alisema Yesu Kristo alikuwa na mwili na upande wa chini tu wa roho (zinapotokea hisia) lakini akili yake ilikuwa ya Kimungu.

Inaonekana alifundisha hivyo katika juhudi za kupinga Uario uliokanusha umungu wa Yesu.Baada ya kupingwa na Theodoreto wa Kuro na Basili Mkuu, fundisho hilo lililaaniwa na Sinodi ya Aleksandria ya mwaka 362, iliyoongozwa na Atanasi wa Aleksandria, na hatimaye kutajwa kama uzushi na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381), uliosisitiza kwamba Kristo ni Mungu kamili na mtu kamili.

Ufalme wa Wavandali

Ufalme wa Wavandali ulienea kwa karne moja (429-534) katika maeneo ya Algeria na Tunisia ya leo, pamoja na kutawala visiwa vya Mediteraneo magharibi.

Hao walikuwa kabila kubwa la Kigermanik la mashariki ambao katika karne tano za kwanza BK walihama kutoka sehemu za Poland ya leo hadi Afrika ya Kaskazini wakiunda ufalme wao.

Wafaranki

Wafaranki walikuwa Wagermanik waliovamia Dola la Roma na hatimaye kujitokeza kama kabila lenye nguvu kuliko yote ya aina hiyo.

Nchi ya Ufaransa imepata jina lake kutoka kwao, ambao waliitawala na kutoka huko wakaeneza himaya yao juu ya sehemu kubwa ya Ulaya Magharibi, wakizuia Waislamu wasiweze kutoka Hispania.

Ushirikiano wao na Mapapa, kama kabila la kwanza la Kijerumani kuingia Kanisa Katoliki bila kupitia kwanza Uario, ni kati ya mambo yaliyoathiri zaidi historia ya Ulaya.

Kilele cha ustawi wao kilifikiwa chini ya mfalme Karolo Mkuu aliyetiwa na Papa Leo III taji la Kaizari wa Roma tarehe 25 Desemba 800. Ndio mwanzo wa Dola Takatifu la Roma.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.