Lugha ya kidini

Lugha ya kidini ni lugha inayotumiwa pekee katika maisha ya kidini kama vile kwa shughuli za liturujia, sala au maandiko matakatifu, wakati wasemaji au wasomaji wa lugha hii ya kidini hutumia lugha nyingine katika maisha ya kawaida.

Devimahatmya Sanskrit MS Nepal 11c
Maandishi ya Kisanskrit yaliyo ya zamani kuliko yote yaliyobaki hadi leo: Devi Māhātmya, juu ya jani la mtende, Bihar au Nepal, karne ya 11.

Lugha za kale kama lugha za kidini

Mara nyingi lugha za kidini ni lugha za kale zinazohifadhiwa katika maisha ya kidini lakini katika maisha ya kawaida zimeshabadilika sana.

Kilatini

Hadi mwaka 1964 ibada karibu zote za Kanisa Katoliki duniani kote ziliendesha kwa lugha ya Kilatini. Mtaguso wa Pili wa Vatikani ulibadilisha utaratibu huo na kupendelea lugha za watu wenyewe zitumike katika ibada. Hata hivyo hadi leo kuna misa na ibada za Kilatini katika makanisa machachechache na monasteri za nchi mbalimbali.

Kislavoni cha Kanisani

Katika Makanisa ya Kiorthodoksi ya Bulgaria, Poland, Serbia na Urusi liturujia za ibada ni kwa lugha ya Kislavoni cha Kanisani. Lugha hiyo inatunza hali ya Kislavoni ya miaka 1000 iliyopita kilichogeuka baadaye kuwa lugha mbalimbali za kisasa.

Asili ni kazi ya watakatifu Methodio na Kyrilo wa Saloniki waliotafsiri vitabu vya Ukristo kwa ajili ya misheni kati ya Waslavoni. Walitumia lugha ya kawaida ya wakati ule mnamo mwaka 800 BK lakini lahaja mbalimbali za Kislavoni zimeendelea kubadilika hadi lugha mpya za Kislavoni zimetokea kama vile Kirusi, Kibulgaria n.k.

Tangu karne nyingi hakuna mtu anayetumia tena kile Kislavoni cha kale kwa maisha ya kila siku, lakini inaendelea kuwa lugha ya ibada na liturujia katika Makanisa ya Kiorthodoksi ya mataifa ya Kislavoni kama vile Warusi, Wabulgaria, au Waserbia.

Kisanskrit

Kisanskrit kilikuwa lugha ya Waaria walioingia Uhindi takriban miaka 1,500 KK kikawa pia lugha ya kuandika maandiko matakatifu ya Ubanyani. Kisanskrit hufundishwa hadi leo lakini lugha za leo zimekuwa tofauti kabisa.

Lugha za kidini zisizotumiwa tena katika maisha ya kila siku

Lugha za kidini zinazoendelea kuzungumzwa au zilizo karibu na lugha hai

Kuna pia lugha hai zinazotumiwa kama lugha za kidini nje ya eneo wanapokaa wasemaji wao. Mara nyingi hata katika lugha hizi za kidini maneno na matamshi yasiyo ya kawaida tena hutunzwa.

Kiarabu na Uislamu

Mfano wake mkuu ni Kiarabu kama lugha ya kidini kati ya Waislamu. Waislamu walio wengi kabisa hawajui Kiarabu. Wasemaji wa Kiarabu ni takriban 20% za Waislamu wote. Kuna Waislamu wengi kidogo waliojifunza viwango mbalimbali vya Kiarabu, kwanza kwa kurudia maneno ya sala na kutaka kujua zaidi. Hata hivyo idadi kubwa ya Waislamu duniani hawajui Kiarabu ila maneno yanayorudiwa mara kwa mara.

Pamoja na hayo Kiarabu cha Qurani na cha sala ni lugha isiyotumiwa tena na watu katika maisha ya kila siku. Hata sehemu kubwa ya Waarabu wanaelewa kisehemu tu. Sarufi ya Kiarabu sanifu cha kimaandishi cha leo ni bado kilekile kama lugha ya Qurani, lakini msamiati umebadilika mno na pia sarufi ya lugha inayozungumzwa.

Mifano ya Kiingereza na Kijerumani

Kwa lugha za Ulaya kama Kiingereza na Kijerumani kuna tafsiri za Biblia zilizoandikwa takriban miaka 400 - 500 iliyopita. Makanisa mengine yanatunza hali hii ya lugha kwa masomo ya Biblia au pia sala kanisani. Hapa maneno ya karne zilizopita yasiyo ya kawaida tena katika maisha ya kila siku bado yanatunzwa. Kwa Kiingereza ni hasa tafsiri ya Mfalme Yakobo (King James) na kwa Kijerumani ni tafsiri ya Martin Luther.

Tabia hizi zinaonekana katika lugha na tamaduni nyingi.

Kiarabu

Kiarabu (ar.: العَرَبِيَّة‎‎, al-ʻarabiyyah, kwa kirefu al-luġatu al-ʿarabiyya ) ni lugha ya Kisemiti inayotumiwa na watu milioni 206 kama lugha ya kwanza na milioni 246 wa ziada kama lugha ya pili. Ilhali kuna lahaja nyingi, Kiarabu sanifu (ar. الفصحى fuṣḥā) ni lugha rasmi ya nchi 22 za Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na ya Mkutano wa Kilele wa Kiislamu na mojawapo ya lugha rasmi za Umoja wa Mataifa. Kuna pia matumizi kama lugha ya kidini katika Uislamu.

Hivyo Kiarabu ni mojawapo ya lugha muhimu sana duniani ikisomwa kwa viwango tofauti na mamilioni ya waumini Waislamu wakielekea kujifunza na kuelewa kitabu cha Korani. Kama lugha ya kidini ina athari na taathira kubwa juu ya lugha nyingi ulimwenguni na juu ya ustaarabu na utamaduni wa watu na makabila tofautitofauti walio Waislamu.

Kiarabu kwa kawaida huandikwa kwa herufi za Kiarabu.

Ni lugha yenye utajiri mkubwa wa misamiati (maneno), ufasaha mkubwa wa misemo na udhibiti mkubwa wa sarufi na nahau.

Ni lugha iliyokusanya aina nyingi za mithali na mafumbo, na ina utamaduni mkubwa wa nyimbo, mashairi na misemo, nayo inakubaliwa na watu wengi duniani kuwa lugha yenye utamu wa matamshi na uzuri wa lafudhi.

Kwa kuwa Qurani Tukufu na Hadithi za Mtume Muhammad na Mashairi ya zama za Ujahili ndio yenye kudhibiti lugha hii isitetereke wala kubadilika na kupotea kama lugha nyingine nyingi, leo, baada ya miaka zaidi ya elfu, imebaki thabiti kama ilivyokuwa wakati ilipoandikwa Qurani, na mabadiliko yoyote yaliyotokea hayana uhusiano na lugha yenyewe ya Kiarabu, bali yana uhusiano na lahaja na vilugha mbalimbali zinazotumika na Waarabu wa sehemu fulani ya nchi au mji. Ama lugha rasmi ya Kiarabu basi imedhibitika kulingana na Qurani na Sunnah, ili maandishi hayo yaendelee kufahamika milele.

Leo, Kiarabu ni lugha ya sita ulimwenguni kwa wingi wa wanayoitumia kila siku katika maisha yao, baada ya Kichina, Kihindi, Kihispania, Kiingereza na Kibengali.

Umuhimu wa lugha hii unazidi kukua kila siku kwa sababu ya kutumika kwenye maeneo ya katikati ya ulimwengu baina ya mabara ya kale (Afrika, Asia na Ulaya) na mabara mapya ya ulimwengu (Amerika ya Kaskazini na Kusini).

Kiebrania

Lugha ya Kiebrania (עברית ‘Ivrit, matamshi ya kisasa ?) ni moja ya lugha za kisemiti na moja kati ya lugha mbili za kitaifa nchini Israel (pamoja na Kiarabu). Ni kati ya lugha za kale zaidi duniani.

Kiebrania kwa kawaida huandikwa kwa herufi za Kiebrania. Mwandiko huu ni wa konsonanti hasa, kwa kuwa mara nyingi vokali haziandikwi kutokana mfumo wa lugha yenyewe.

Kiebrania ni lugha iliyotumika kuandikia Torati na sehemu kubwa ya maandiko mengine ya Biblia ya Kiebrania. Sehemu hiyo ya Kiebrania pamoja na sehemu ndogo ya Kiaramu huitwa "Tanakh" katika mapokeo ya Kiyahudi na imo katika Agano la Kale ya Biblia ya Kikristo.

Kilatini

Kilatini ni lugha ya kihistoria ambayo siku hizi haina tena wasemaji kama lugha ya kwanza, lakini bado hufundishwa katika shule na vyuo na hata kutumiwa kama lugha ya pili. Ilikuwa pia lugha ya kimataifa ya elimu na istilahi nyingi za kisayansi zimetoka katika Kilatini.

Kilatini kilikuwa lugha hai takriban kati ya miaka 500 KK na 600 BK na baadaye lahaja zake mbalimbali ziliendelea na kukomaa kuwa lugha za pekee zinazojulikana kama lugha za Kirumi.

Kilatini ni pia jina la mwandiko au aina ya herufi (alfabeti ya Kilatini) inayotumika kwa lugha nyingi duniani. Hata Kiswahili huandikwa siku hizi kwa herufi za Kilatini kama kwa mfano ukurasa huu wa Wikipedia.

Kilikuwa

lugha ya Dola la Roma (angalia pia Roma ya Kale)

lugha mama ya lahaja zilizoendelea kuwa lugha za Kirumi kama Kiitalia, Kifaransa, Kihispania, Kireno, Kiromania n.k.

lugha ya elimu na sayansi katika Ulaya kwa karne nyingi

lugha rasmi ya serikali katika nchi nyingi za Ulaya kati ya mwisho wa Dola la Roma mwaka 476 BK hadi mnamo 1700 BK

lugha pekee ya liturgia katika Kanisa la Kilatini hadi mwaka 1965Hadi leo ni

lugha ya kidini katika Kanisa Katoliki

lugha rasmi katika nchi ya Vatikano.

Kilatini ina athira kubwa katika lugha ya sayansi na elimu. Hadi leo hufundishwa mashuleni hasa Ulaya.

Kiswahili kimerithi maneno yenye asili ya Kilatini hasa kupitia Kiingereza kilichopokea karibu asilimia hamsini ya maneno yake yote kutoka Kilatini kupitia hasa Kifaransa. Maneno mengine ya Kilatini yameingia Kiswahili kupitia Kireno, Kifaransa n.k.

Kilatini huendelezwa na kukuzwa na wapenzi wa lugha. Kuna misamiati ya "Kilatini cha Kisasa" yenye maneno kwa ajili ya mitambo ya kisasa, mtandao n.k. Wikipedia ya Kilatini ilifikia makala zaidi ya 130,000 kwenye mwaka 2019.

Mwandiko wa Kiebrania

Mwandiko wa Kiebrania ni mwandiko au alfabeti ya lugha ya Kiebrania ya kale na ya kisasa, pia ya Kiaramu ya Biblia na ya Talmudi.

Kuna pia lugha nyingine za Kiyahudi kama Kiyiddish na Kiladino zilizoandikwa kwa kutumia mwandiko huu.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.