Lugha

Lugha (kutoka neno la Kiarabu: لغة) ni utaratibu wa kuwasiliana kati ya binadamu (wengine wanadai hata kati ya viumbe wenye akili).

Somo la lugha linaitwa maarifa ya lugha au isimu.

Mwaka wa 2008 ulikuwa Mwaka wa Lugha wa Kimataifa.

ASL family
Mawasiliano kwa lugha ya ishara ya Kimarekani

Maana ya neno "lugha"

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu zenye maana na zilizokubaliwa na jamii ya watu fulani ili zitumike katika kuleta mawasiliano.

Lugha ni mfumo wa sauti za nasibu kwa sababu zilitokea kama bahati tu kwa binadamu. Wanyama hawatumii lugha kama chombo cha mawasiliano, kwa kuwa lugha ni sauti zenye maana na kukubaliwa na jamii.

Hakuna lugha bora zaidi duniani, kwa kuwa lugha zote zina ubora, mradi zikidhi matakwa ya jamii husika.

Mbali na maana ya kawaida kuna pia lugha ya ishara inayotumiwa na watu bubu. Katika fani ya programu za kompyuta ni kawaida kuongea juu ya "lugha ya kompyuta".

Umuhimu wa lugha

 • Lugha ni kitambulisho cha jamii
 • Lugha hutolea elimu
 • Lugha huleta mawasiliano katika jamii
 • Lugha hukuza utamaduni
 • lugha huburudisha

Tabia za lugha

Lugha huwa na tabia zifuatazo:

 • Lugha huzaliwa: ni kutokana na lugha nyingine moja au zaidi zilizotangulia kuwepo.
 • Lugha hukua: lugha hukua (kuongezeka kwa maneno, kuongezeka kwa idadi ya wazungumzaji, kuwa na mawanda mapana, kusanifiwa) kadiri inavyoendelea kutumiwa na jamii.
 • Lugha hutohoa: lugha ina tabia ya kuchukua au kukopa maneno kutoka lugha nyingine.
 • Lugha hufundishika: mtu yeyote anaweza kujifunza walau kiasi lugha yoyote hata kwa njia ya ufundishaji.
 • Lugha huathiriana: lugha yoyote inaweza kuathiriwa na lugha nyingine.
 • Lugha lazima ijitosheleze: kila lugha inajitosheleza kulingana na mahitaji ya jamii inayotumia lugha yenyewe.
 • Lugha zina ubora: lugha zote ni bora hakuna lugha bora kuliko nyingine zote.
 • Lugha hurithiwa: jamii hurithi lugha kutoka kizazi hadi kizazi.
 • Lugha hufa: inapozidi mno kubadilika mwisho si yenyewe tena, lakini pia inapoachwa isitumike tena kwa kuwa wahusika wanapendelea lugha nyingine.

Sifa za lugha

 • Lugha lazima iwe inahusu binadamu
 • Sauti-sauti hufanywa na mwanadamu
 • Lugha hufuata misingi ya fonimu, yaani, a, b, ch, d, f, h, z n.k.
 • Lugha huwa na mpangilio maalumu wenye kubeba maana. Mpangilio huo huanza na fonimu ---> Silabi ---> Neno
 • Lugha hujitambulisha ili kuzalisha maneno mengi.

Dhima za lugha

 1. Lugha hutumika kama chombo cha mawasiliano kwa kupashiana habari.
 2. Lugha hutumika kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano miongoni mwa wanajamii.
 3. Lugha hutumika kutunza, kukuza, na kuendeleza utamaduni wa jamii.
 4. Lugha hutumika katika kutetea maarifa mbalimbali (ni nyenzo ya kufundishia).
 5. Lugha hutumika kama alama ya utambulisho wa kabila/jamii au taifa fulani.
 6. lugha hutumika kutoa burudani.

Aina za lugha kwa kigezo cha uwasilishaji

Kimsingi lugha ni moja. Uwasilishwaji wake ndio huigawa katika tanzu/aina kuu mbili:

 1. Lugha ya mazungumzo
 2. Lugha ya maandishi

Lugha ya mazungumzo

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa na watu kwa njia ya mazungumzo ya mdomo - na hurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa njia ya mazungumzo. Lugha ya mazungumzo ni kongwe, hai na halisi zaidi ya mzungumzaji na ina maana nyingi, kwani mzungumzaji na msikilizaji huwa ana kwa ana katika mazingira mamoja.

Stadi za lugha ya mazungumzo ni kuzungumza na kusikiliza.

Na. Chanzo Kikomo
1 Kuzungumza Kusikiliza
2 Mzungumzaji Msikilizaji

Lugha ya maandishi

Hii ni lugha ambayo huwasilishwa kwa njia ya maandishi. Hii ni kiwakilishi cha lugha ya mazungumzo katika mfumo wa maandishi. Lugha ya maandishi ni changa kwani imeanza milenia za hivi karibuni baada ya kuvumbuliwa kwa maandishi.

Stadi za lugha ya maandishi ni kuandika na kusoma:

Na. Chanzo Kikomo
1 Kuandika/Maandishi Kusoma
2 Mwandishi Msomaji

Kwa kawaida, lugha ni sehemu ya utamaduni wa umma fulani. Lugha ya aina hii inaitwa lugha asilia. Lakini pia kuna lugha za kuundwa.

Nyanja za lugha

Lugha ina nyanja kuu mbili, nazo ni:

 • Sarufi - hushughulikia kanuni za lugha
 • Fasihi - hushughulikia sanaa zitokanazo na lugha husika ili kuumba kazi mbalimbali za kifasihi.

Kukua na kufa kwa lugha

Tangu siku za kwanza za binadamu, lugha zimekuwa zikichipuka, kukua, kutangaa na kufa kama kiumbe yeyote mwingine. Kwa hivyo, lugha zilizopo leo ulimwenguni, huenda baada ya karne nyingi kupita zikatoweka na kuzuka nyinginezo.

Leo ulimwenguni mathalan, kuna lugha karibu 6,700, zikiwa 1,000 katika bara la kaskazini na la kusini la Amerika, 2,000 zikiwa kwenye bara la Afrika, 230 katika bara la Ulaya, 2,200 katika bara la Asia, na 1,300 katika bara la Oshania (Australia na nchi jirani nayo).

Kurasa zinazohusiana

Tazama pia

 • Lango la lugha

Viungo vya nje

Afrika

Afrika ni bara la pili duniani kwa ukubwa, likiwa na eneo la kilometa za mraba zipatazo 30,370,000 na kwa idadi ya wakazi, hao wakiwa 1,225,080,510 (mwaka 2016). Asia ndiyo bara pekee la kushinda Afrika.

Bahari ya Mediteranea

Bahari ya Mediteranea (pia: Bahari ya Kati) ni bahari ya pembeni ya Atlantiki kati ya mabara ya Afrika, Ulaya na Asia ya Magharibi. Eneo lake ni takriban milioni 2,5 km². Kina chake kirefu ni 5,267 m. Ina kanda ya hali ya hewa ya pekee pamoja na mimea na wanyama.

Neno "Mediteranea" limetokana na lugha ya Kilatini likiunganisha maneno ya "medium" (inamaanisha "kati ya, katikati") na "terra" (inamaanisha "bara"). Kwa hiyo neno lenyewe linamaanisha "Bahari katikati ya bara".

Katika lugha ya Biblia Kiebrania iliitwa "Bahari ya Magharibi" au "Bahari Kuu"; Waroma wa Kale waliotwala nchi zote zinazopakana na Bahari ya Mediteranea waliita "mare nostrum" yaani "bahari yetu". Waarabu na Waturuki wanaiita "Bahari Nyeupe" (kwa Kituruki: Akdeniz; kwa Kiarabu: البحر الأبيض al-baHr-al-abyaD)

Kifaransa

Kifaransa (kwa Kifaransa: français) ni lugha ya Ufaransa (pamoja na maeneo yake ya ng'ambo), Ubelgiji ya Kusini, Uswisi ya Magharibi, Luxemburg na Kanada. Inazungumzwa pia katika nchi nyingi za Afrika kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Senegal, Mali, Shelisheli, Chad, n.k., Asia ya Kusini na Amerika zilizokuwa koloni za Ufaransa.

Kiingereza

Kiingereza ni lugha ya jamii ya Kigermanik cha Magharibi iliyokua nchini Uingereza kwa muda wa miaka 1,400.

Leo, zaidi ya wasemaji milioni mia nne duniani wanazumgumza Kiingereza kama lugha ya kwanza. Watu wengi zaidi wanazumgumza Kiingereza kama lugha ya pili, kwa sababu ni muhimu sana kwenye nyanja za mawasiliano, sayansi na uchumi wa kimataifa.

Kiswahili

Kiswahili ni lugha ya Kibantu yenye misamiati mingi ya Kiarabu (30%), lakini sasa ya Kiingereza pia (10%), inayozungumzwa katika eneo kubwa la Afrika ya Mashariki.

Lugha hii ina utajiri mkubwa wa misamiati, misemo, methali, mashairi, mafumbo, vitendawili na nyimbo. Kiswahili hutumika kufundishia shuleni na kuna vitabu vingi vilivyotungwa kwa kutumia lugha hiyo, vikiwa pamoja na vile vya hadithi, hekaya au riwaya.

Lugha za Kiaustronesia

Lugha za Kiaustronesia ni familia ya lugha ambazo huzungumzwa katika visiwa vya Pasifiki, vya Asia ya Kusini-Mashariki na kisiwa cha Madagaska. Katika familia hiyo kuna lugha zaidi ya 1200 zenye wasemaji milioni 386. Lugha ya Kiaustronesia yenye wasemaji wengi mno ni Kimalay ambayo huzungumzwa na watu milioni 180.

Marekani

Muungano wa Madola ya Amerika (kwa Kiingereza: United States of America), inajulikana pia kama Marekani (kwa Kiingereza: United States, US, USA au America), ni nchi inayopakana na Kanada na Meksiko katika Amerika ya Kaskazini, mbali ya kuundwa pia na visiwa vya Hawaii.

Mji mkuu wa Marekani ni Washington DC.

Mkoa wa Kaskazini, Uganda

Mkoa wa Kaskazini ni mmoja wa mikoa (kwa Kiingereza: regions) minne ya Uganda.

Wakati wa sensa ya mwaka 2014 Mkoa wa Kaskazini ulikuwa na wakazi 7,188,139. Sawa na mikoa mingine Mkoa wa Kaskazini hauna mamlaka ya kiutawala.

Mto Kiama

Mto Kiama unapatikana Kenya. Ni tawimto la mto Thika, ambao tena ni tawimto la mto Tana ambao ndio mrefu kuliko yote nchini na unaishia katika Bahari ya Hindi.

Mto Lumi

Majiranukta kwenye ramani: 3°32′44″S 37°45′17″E

Mto Lumi (au Lomi au Luffu) ni mmojawapo kati ya mito ya Tanzania (upande wa kaskazini mashariki) na ya Kenya (upande wa kusini).

Unatiririka hadi ziwa Jipe.

Tanzania

Tanzania ni nchi iliyoko Afrika ya Mashariki.

Imepakana na Uganda na Kenya upande wa kaskazini, Bahari Hindi upande wa mashariki, Msumbiji, Malawi na Zambia upande wa kusini, Kongo, Burundi na Rwanda upande wa magharibi.

Eneo lina kilometa za mraba 947,303 (nchi ya 31 duniani); maji ya ndani yanachukua asilimia 6.2.

Idadi ya watu kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 ilikuwa 44,928,923 (nchi ya 30 duniani) kutoka 34,443,603 waliohesabiwa katika sensa ya mwaka 2002.

Msongamano ni wa watu 47.5 kwa km² (nchi ya 124 duniani).

Tanzania ni nchi kubwa zaidi kati ya wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki.

Mji mkuu ni Dodoma (wenye wakazi 410,956), lakini rais bado yupo Dar es Salaam, jiji kubwa zaidi, lenye watu zaidi ya milioni 4,364,541.

Miji mingine ni kama vile Mwanza (706,543), Arusha (416,442), Mbeya (385,279), Morogoro (315,866), Tanga (273,332), Kahama (242,208), Tabora (226,999) na Zanzibar (223,033).

Thika (mto)

Mto Thika unapatikana katika kaunti ya Kiambu katikati ya Kenya.

Ni tawimto la mto Tana ambao ndio mrefu kuliko yote nchini na unaishia katika Bahari ya Hindi.

Mto Thika ni chanzo cha nishati ya maji, na pia hutoa maji kwa Nairobi, mji mkuu wa Kenya.

Jina la Thika halijulikani kama limetoka lugha ya Kikuyu ama lugha ya Kimaasai. Katika Kikuyu, guthika maana yake kuzika; na katika Kimaasai, jina linafanana na sika maana yake kusugua ukingoni.

Tovuti

Tovuti ni mkusanyiko wa kurasa zilizoandikwa kwa lugha mbalimbali za tarakilishi kama vile HTML, PHP, XHTML na kadhalika na ambazo kwa pamoja hujumuika katika kutoa habari au maelezo kuhusu jambo fulani. Lugha hizi, yaani HTML, PHP, XHTML na kadhalika zinaweza tu kusomwa na kutafsiriwa na programu kama vile Internet Explorer Google Chrome na Mozilla Firefox kwa lugha ambayo inaweza kueleweka na binadamu. Wingi wake ni "tovuti" vile vile. Tovuti zote pamoja zinaitwa "mtandao" au "Intaneti" au "wavuti".

Ufaransa

Ufaransa ni nchi ya Ulaya na mwanachama mwanzilishi wa Umoja wa Ulaya.

Mji mkuu ni Paris.

Eneo lake ni km² 674,843; na idadi ya wakazi ni 63,044,000.

Imepakana na Ubelgiji, Luxemburg, Ujerumani, Uswisi, Italia, Monako, Andorra na Hispania.

Ufaransa ulikuwa kati ya nchi zenye makoloni mengi ikasambaza lugha yake kote duniani na kutunza uhusiano wa pekee na nchi nyingine zinazotumia Kifaransa.

Uganda

Uganda ni nchi ya Afrika ya Mashariki. Imepakana na Kenya upande wa mashariki, Sudan Kusini upande wa kaskazini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo upande wa magharibi, Rwanda na Tanzania upande wa kusini.

Uganda inamiliki sehemu ya ziwa la Viktoria Nyanza ikipakana huko na Kenya na Tanzania.

Uganda ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki na wa miundo mingine mbalimbali ya kimataifa.

Uingereza

Uingereza (pia: Ingilandi kutoka Kiingereza: England) ni nchi kubwa ndani ya Ufalme wa Muungano yenye wakazi milioni 50 (83% ya wakazi wote wa Ufalme) na eneo lake ni takriban km² 130,000 (theluthi mbili za kisiwa cha Britania).

Ujerumani

Ujerumani (pia: Udachi, kwa Kijerumani: Deutschland) ni nchi ya Ulaya ya Kati.

Imepakana na Denmark, Poland, Ucheki, Austria, Uswisi, Ufaransa, Luxemburg, Ubelgiji na Uholanzi.

Ni nchi yenye watu wengi katika Ulaya, isipokuwa Urusi ina watu zaidi.

Uchumi wa Ujerumani una uwezo mkubwa: ni nchi inayouza bidhaa nyingi nje kushinda mataifa yote ya dunia.

Muundo wake kiutawala ni shirikisho la jamhuri lenye majimbo 16 ndani yake na kila jimbo lina kiwango cha kujitawala.

Uturuki

Uturuki (Jamhuri ya Uturuki; kwa Kituruki: Türkiye Cumhuriyeti) ni nchi ya kimabara kati ya Asia na Ulaya.

Sehemu kubwa iko Asia ya magharibi lakini sehemu ndogo ya eneo lake upande wa magharibi wa Bosporus iko Ulaya.

Wikimedia Commons

Wikimedia Commons (pia huitwa "Wikicommons") ni hazina ya kuhifadhia na kutumia faili za picha, za sauti na nyinginezo.

Utumiaji wa faili hizo ni huru kwa wikipedia za lugha zote; tena si lazima kuzipakia kwenye wikipedia mojamoja kwa vile zinapatikana kutoka wikipedia zote.

Wikimedia Commons ni mradi wa Wikimedia Foundation.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.