Kutoka (Biblia)

Kitabu cha Kutoka ni kitabu cha pili katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania), na kwa hiyo pia katika Agano la Kale (sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo); kitabu cha kwanza ni Mwanzo.

Kwa asili kimeandikwa kwa Kiebrania, na katika lugha hiyo kinaitwa שמות, Shemot, maana yake “majina”, kutokana na neno lake la kwanza.

Wengine wanakiita Kitabu cha Pili cha Mose (au Musa) kwa vile inafikiriwa kuwa ndiye mwandishi wa kitabu hicho. Kwa lugha ya Kiyunani, kinaitwa ἔξοδος, Exodos, maana yake “kuondoka kwa watu wengi pamoja”.

Kitabu cha Kutoka kina sura arobaini.

  • Sura 1 hadi 18 zinasimulia Waisraeli walivyokombolewa na Mungu kutoka utumwani kule Misri na walivyosafiri mpaka Mlima Sinai.
  • Sura 19 hadi 24 zinasimulia Mungu alivyofanya nao agano pamoja na kuwapa mwongozo wa maisha (Amri Kumi na maagizo mengine).
  • Sura 25 hadi 31 zinaeleza utengenezaji wa hema takatifu (au hema la mkutano) na Sanduku la Agano.
  • Sura 32 hadi 34 zinahadithia Waisraeli walivyoasi na kuabudu sanamu ya ndama wakati Mose alipokuwa amekwenda kuzungumza na Mungu mlimani Sinai.
  • Hatimaye, sura 35 hadi 40 zinaeleza maagizo mengine kuhusu hema takatifu.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

The Crossing fo The Red Sea
"Kuvuka Bahari ya Shamu" kadiri ya Nicholas Poussin.
Rembrandt Harmensz. van Rijn 079
Mose akishika mbao za Amri Kumi (mchoro wa Rembrandt, 1659).

Utangulizi

Kama ilivyokuwa kwa kitabu cha Mwanzo, hata kitabu cha Kutoka kilipewa jina jipya na watafsiri wa kwanza wa Biblia ya Kiebrania (Agano la Kale) katika lugha ya Kiyunani (tafsiri ya Septuaginta). Maana ya jina hilo ni 'kutoka nje' au 'kuhama', kwa kuwa kitabu kinaeleza habari za kutoka au kuhama Misri.

Habari za kitabu cha Mwanzo zilimalizika kwa familia ya Yakobo-Israeli) kuhamia nchi ya Misri. Kitabu cha Kutoka kinaanza habari zake muda wa miaka kama 400 hivi baada ya hayo (Mwa 15:13; Kut 12:41).

Wakati huo wazao wa Israeli walikuwa wameongezeka sana, hata walikuwa taifa la maana, ingawa bado waliishi Misri. Kitabu hiki kinaonyesha jinsi Mungu alivyowaokoa katika utumwa wa Misri, akawapeleka mpaka karibu na Mlima Sinai, na huko alithibitisha rasmi agano alilolifanya na Ibrahimu, ili Israeli liwe kweli taifa na mali ya Mungu, nalo liishi kwa ajili yake. Kisha Mungu, kwa njia ya Musa, aliwapa watu hao kanuni zile ambazo kwa njia yake waishi, pia aliwapa sheria za dini walizotakiwa kuzitimiza ili kufurahia na kufaidi baraka za agano.

Ufunuo wa tabia ya Mungu

Licha ya thamani yake ya kutoa masimulizi ya matukio ya historia ambayo maisha ya kidini na ya kijamii ya Israeli yalijengwa juu yake, kitabu cha Kutoka pia kina thamani katika kudhihirisha sehemu kubwa ya tabia ya Mungu wa Israeli. Zaidi ya yote, alidhihirishwa kuwa Mungu aokoaye. Waisraeli walitakiwa wamkumbuke daima kuwa ndiye aliyewaokoa na kuwatoa 'katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa' (Kut 6:3-8; 20:2).

Waisraeli walitakiwa watambue historia yao si kama kusanyiko la masimulizi ya matukio, bali kama ufunuo wa tabia ya Mungu. Yeye kwao alikuwa nani, aliwafanyia nini, naye aliwatazamia wafanye mambo gani?

Mungu alishughulika na kila sehemu ya maisha wa Waisraeli. Matendo yake ya kuokoa yalikuwa yenye ushindi, na hukumu zake ziliangamiza. Kuhifadhiwa kwa taifa na kukua kwake kulikuwa kazi yake (Kut 1:21; 14:21-22:31; 32:35).

Mungu wa Israeli pia alikuwa Mtakatifu, maana yake watu wake pia wawe watakatifu. Walitakiwa wawekwe wakfu kwa Mungu, wakifuata kwa uangalifu sana matakwa yake kuhusu maisha ya maadili yaliyopangwa wazi naye (Kut 19:5).

Hata hivyo, Mungu huyo aliyetofautiana kabisa na wanadamu wenye dhambi (Kut 19:12-13), pia alitaka kuishi kati ya watu (Kut 25:8; 33:14). Yule ambaye utakatifu na [[haki] yake vilidai adhabu na hukumu kwa wenye dhambi (Kut 32:33), alikuwa yuleyule ambaye kwa huruma na neema yake aliandaa njia kwa wenye dhambi ili waweze kumkaribia tena, wasamehewe dhambi zao na kurudishwa tena katika ushirika hai na Mungu Mtakatifu (Kut 29:10-14; 34:6-7).

Muhtasari

1:1-4:31 Maandalizi ya Musa

5:1-15:21 Kuokolewa kutoka Misri

15:22-18:27 Safari ya kwenda Sinai

19:1-24:18 Kutolewa kwa agano

25:1-31:18 Hema la kukutania na ukuhani

32:1-34:35 Kuvunjwa kwa agano na matengenezo yake

35:1-40:38 Kuandaliwa na kujengwa kwa hema la kukutania

Marejeo

Vitabu vya ufafanuzi

  • Fretheim, Terence E (1991). Exodus. Westminster John Knox Press.
  • Meyers, Carol B (2005). Exodus. Cambridge University Press.
  • Stuart, Douglas K (2006). Exodus. B&H Publishing Group.

Vingine

Viungo vya nje

Mwanzo Kutoka Walawi Hesabu Kumbukumbu Yoshua Waamuzi Ruthu Samueli I Samueli II Wafalme I Wafalme II Mambo ya Nyakati I Mambo ya Nyakati II Ezra Nehemia TobitiDK YudithiDK Esta Wamakabayo IDK Wamakabayo IIDK Yobu Zaburi Methali Mhubiri Hekima DK SiraDK Wimbo Bora Isaya Yeremia Maombolezo BarukuDK Ezekieli Danieli Hosea Yoeli Amosi Obadia Yona Mika Nahumu Habakuki Sefania Hagai Zekaria Malaki - Alama ya DK inaonyesha vitabu vya deuterokanoni visivyopatikana katika matoleo yote ya Biblia.

Kesha

Kesha au Mkesha (kwa Kiingereza Vigil, kutoka Kilatini vigilia, yaani hali ya kuwa macho) ni kipindi cha kutolala kwa makusudi, hasa kwa lengo la kidini, kama vile kusali kirefu.

Mara nyingi kesha linafanyika kabla ya adhimisho maalumu, kama vile sikukuu fulani, lakini kuna waumini, hasa watawa, wanaokesha kila usiku walau kwa muda fulani.

Nje ya dini, makesha yanafanyika hasa kandokando ya mgonjwa aliye mahututi na ya maiti ya marehemu.

Kiongozi Kalenda

Kiongozi Kalenda ni kijitabu chenye chaguo cha maneno kutoka Biblia kwa kujisomea kila siku. Maneno haya hutazamiwa kama "maneno ya mwongozo wa kiroho" kwa ajili ya siku husika. Hutolewa na Kanisa la Moravian katika nchi nyingi duniani kwa lugha zisizopungua 50. Jina lake la Kiingereza ni "Daily Watchwords" na kwa Kijerumani "Losungen". Hutolewa upya kila mwaka.

Kipindi cha masomo

Kipindi cha masomo (kwa Kilatini "Officium lectionis") ni kipindi muhimu cha Sala ya Kanisa katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo.

Ni sala rasmi ambayo kwa asili inafanyika wakati wa usiku: ama usiku kati ama kabla ya pambazuko ili kumtolea Mungu sifa na dua pamoja na kutafakari Neno lake katika utulivu wa hali ya juu.

Katika utaratibu wa Kanisa la Roma, unaofuatwa na majimbo karibu yote ya Kanisa Katoliki la Kilatini, sehemu kuu za sala hiyo, kati ya utangulizi na baraka ya mwisho, ni utenzi, zaburi tatu (au vipande vitatu vya Zaburi), kiitikizano kifupi, somo refu kutoka Biblia ya Kikristo, kiitikizano kirefu, somo refu kutoka maandishi ya Kikristo (hasa ya Mababu wa Kanisa), kiitikizano kirefu na sala ya kumalizia.

Katika siku muhimu zaidi baada ya masomo na viitikizano kuna utenzi mwingine mrefu, maarufu kwa maneno yake ya kwanza katika Kilatini, "Te Deum".

Wanaopenda kurefusha sala hiyo katika kukesha wanaweza wakaongeza zaburi nyingine tatu (au vipande vitatu vya Zaburi) kati ya masomo hayo mawili, halafu nyimbo tatu kutoka Agano la Kale na somo la Injili.

Korintho

Korintho (kwa Kigiriki: Κόρινθος, Kórinthos) ni mji wa Ugiriki wa Kusini. Uko kwenye shingo ya nchi ya Korintho inayounganisha rasi ya Peloponesi na sehemu kubwa ya Ugiriki bara.

Siku hizi ni mji mdogo tu, wenye wakazi 36,555, lakini ina historia kubwa na ndefu.

Kimataifa Korintho inajulikana kutokana na mfereji wa Korintho unaokata shingo ya nchi kwa urefu wa kilomita sita na kufupisha safari kutoka bahari ya Adria kuingia Mediteranea ya mashariki kwa meli ndogo na za wastani.

Kihistoria jina la mji linajulikana zaidi kutoka Biblia ya Kikristo, na hasa barua za Mtume Paulo kwa Wakristo mjini zinazopatikana katika Agano Jipya kama Waraka wa kwanza kwa Wakorinto (1Kor) na Waraka wa pili kwa Wakorinto (2Kor).

Liturujia ya Kimungu

Liturujia ya Kimungu ni adhimisho la ekaristi kwa jina linalotumiwa hasa na Waorthodoksi na Wakatoliki wa Mashariki wanaofuata madhehebu ya Kigiriki.

Ina sehemu kuu mbili: moja ambayo inaruhusu wakatekumeni kuhudhuria, ya pili ni kwa ajili ya waamini waliobatizwa tu.

Masifu ya asubuhi

Masifu ya asubuhi ni kipindi muhimu cha Sala ya Kanisa katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo, kwa kuwa kinaonyesha kwamba sala ndiyo kazi ya kwanza ya binadamu siku yoyote.

Ni sala rasmi inayofanyika wakati wa jua kupambazuka ili kumtolea Mungu sifa kwa siku mpya inayoanza, ambayo inadokeza pia ufufuko wa Yesu.Katika utaratibu wa Kanisa la Roma, unaofuatwa na majimbo karibu yote ya Kanisa Katoliki la Kilatini, sehemu kuu za sala hiyo, kati ya utangulizi na baraka ya mwisho, ni utenzi, zaburi moja (au kipande chake) inayotaja asubuhi, wimbo kutoka Agano la Kale, zaburi nyingine ambayo daima ni ya kusifu Mungu, somo fupi au refu kutoka Biblia ya Kikristo, kiitikizano, wimbo wa Zakaria, maombi, Baba Yetu na sala ya kumalizia.

Kati ya sehemu hizo, kilele ni maneno ya Injili (wimbo wa Zakaria na Baba Yetu).

Meriba

Meriba (kwa Kiebrania מְרִיבָה, Meribah, "masutano") ni kituo kimojawapo cha safari ya Waisraeli kutoka Misri hadi Kanaani chini ya Musa ambayo inasimuliwa kirefu na Torati (Kut 17:7; Hes 20:13). Katika Kutoka (Biblia), Meriba inatajwa pia kama Masa, ingawa madondoo mengine yanadokeza kwamba ni mahali tofauti (k.mf. Kumb 33:8)Inaonekana huko Waisraeli walimlalamikia kiongozi wao na hivyo Mungu pia kuhusu maji waliyoyakosa kwa ajili yao na ya mifugo yao. Kwa sababu hiyo, imechukuliwa kama kielelezo cha kumjaribu Mungu kwa utovu wa imani, hasa kwa kuwa kweli maji yalipatikana kimuujiza kutoka mwambani.

Kadiri ya Hesabu (Biblia) 20:12, hata Musa na kaka yake Haruni walikosa imani huko hata wakaadhibiwa kwa kunyimwa fadhili ya kuingia Nchi ya ahadi.

Kwa sababu hiyo pia, kwanza Zaburi (Biblia) 95, halafu Waraka kwa Waebrania 3-4, vinaonya wote kuwa na imani kila siku, si kumjaribu Mungu.

Kadiri ya Kutoka, mahali ni karibu na Refidim, kituo cha mwisho kabla ya Mlima Sinai, lakini kadiri ya Hesabu ni kaskazini zaidi, karibu na Kadeshi.

Misale

Misale, katika Kanisa Katoliki la Magharibi, ni kitabu cha liturujia kinachokusanya yale yanayohitajika kuadhimishia Misa (matini ya sala na nyimbo, pamoja na taratibu za vitendo mbalimbali n.k.).

Missale plenum (yaani Misale kamili) ilitokea katika Kanisa la Kilatini kwenye karne XI ili kukusanya pamoja yaliyokuwemo katika vitabu mbalimbali vilivyohitajika kwa Misa: Sakramentari yenye sala, Kitabu cha Injili, Kitabu cha masomo mengine kutoka Biblia, Graduale yenye nyimbo.

Missale plenum ilienea kote kati ya karne XIII na ile ya XV.

Baada ya Mtaguso wa pili wa Vatikano, masomo yaliondolewa katika Misale na kurudishwa katika vitabu tofauti vya kutumiwa kwenye mimbari, wakati Misale inatakiwa kutumika kwenye kiti cha padri na altareni.

Misale ya waumini

Misale ya waumini ni kitabu kidogo ambacho kinawaletea Wakatoliki wanaotumia lugha ya Kiswahili matini ya sala na masomo kutoka Biblia ya Kikristo kadiri ya utaratibu wa Misa za Jumapili na sikukuu za kalenda ya liturujia ya mapokeo ya Kiroma.

Mbali na hayo, yanayotokana na vitabu rasmi vya Misale ya altare na Kitabu cha masomo, katika kitabu hicho waumini wanakuta pia sala na ibada nyingine za binafsi.

Ndiyo sababu misale hiyo imetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania mara nyingi na kusambaa nchini kote na hata nje yake.

Nevertheless (bendi)

Nevertheless, mara nyingi hufupishwa kuwa NTL, ni bendi la Kikristo linaloimba nyimbo za mtindo wa pop linalotoka eneo la Chattanooga, Tennessee. Wimbo wao "Live Kama We're Alive" ulifika nafasi ya tano kwenye chati ya nyimbo za Kikristo ya R&R Christian Rock Chart. Wimbo wao wa "The Real," ulichezwa sana katika stesheni za redio za Kikristo zinazochezesha nyimbo za kisasa. The Real ulikuwa katika chati nyingi za Nyimbo Bora Kumi kote nchini Marekani. Bendi hili lilitangaza uamuzi wao wa kustaafu na wakashiriki katika tukio lao la mwisho mnamo Desemba 2009. Walitoa uamuzi huu kwa sababu ya maisha ya kibinafsi na pia shinkizo kutoka watu wengine.

Bendi hili limezuru na mabendi mengine mengi yanayoimba nyimbo za Kikristo za kisasa kama vile : Superchick, Skillet, Hawk Nelson, Falling Up, na Number One Gun.

Sala ya moyo

Sala ya moyo ni aina mojawapo ya sala isiyohitaji kutoa sauti na pengine hata kupanga mawazo namna inayofanyika katika tafakuri.

Makala hii inategemea hasa mang'amuzi ya Wakristo, hususan Wakatoliki.

Torati

Torati (kwa Kiebrania: תורה, Torah), maana yake ni fundisho, mwongozo au sheria. Kwa jina hilo vinatajwa kwa pamoja vitabu vitano vya kwanza vya Tanakh, vinavyojulikana pia kwa jina lenye asili ya Kigiriki la Pentateuko (pente maana yake tano, teukhos maana yake kitabu).

Kwa jina hilohilo Wayahudi wanamaanisha pia sheria ya dini yao kwa jumla, wakitofautisha Torah shebiktav (sheria iliyoandikwa yaani vitabu hivyo vitano) na Torah shebehalpeh kwa mapokeo yote yaliyokubalika baadaye.

Kusoma Torah ni wajibu muhimu mmojawapo wa kila Mwisraeli. Ni desturi kusoma Torati nzima kwa mwaka mmoja, na kwa ajili hiyo imegawiwa katika sehemu 54 (parashoth, wingi wa parasha, yaani "sehemu"), kama zilivyo siku za Sabato katika miaka mirefu (yenye miezi 13).

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.