Kigiriki

Kigiriki (pia: Kiyunani) ni lugha ya Kihindi-Kiulaya inayotumiwa hasa nchini Ugiriki. Maandishi yake yamejulikana tangu miaka 3500 iliyopita. Hakuna lugha nyingine duniani inayozungumzwa hadi leo yenye historia ndefu kuliko hii, isipokuwa Kichina.

Kigiriki ni muhimu sana kwa utamaduni wa kisasa kwa sababu ya kutoa michango mingi kwa lugha ya sayansi, teknolojia na utamaduni. Fikra nyingi muhimu zilionekana mara ya kwanza kwa Kigiriki na falsafa iliyojadiliwa na kuandikwa kwa lugha hii. Istilahi nyingi za kisayansi zimetoka katika Kigiriki.

Alfabeti ya Kigiriki ilikuwa msingi wa alfabeti nyingine mbili, za Kilatini na Kikirili, pia kwa miandiko ya abijadi kama herufi za Kiarabu au za Kiebrania. Kiswahili huandikwa leo kwa herufi za Kilatini.

Kati ya maandiko muhimu ya Kigiriki ni yale ya wanafalsafa kama Plato na Aristoteles na pia baadhi ya maandiko ya Biblia ya Kikristo (Agano Jipya pamoja na Deuterokanoni), mbali ya tafsiri ya kwanza ya Biblia ya Kiebrania maarufu kwa jina la Septuaginta (karne ya 2 KK).

Kati ya karne ya 3 KK hadi karne ya 6 BK Kigiriki kilikuwa lugha ya kimataifa katika eneo kubwa la kandokando ya bahari ya Mediteranea pamoja na Mashariki ya Kati.

Lugha imeendelea kubadilika kisarufi, kimatamshi na pia kimsamiati. Hivyo Kigiriki cha kale kimekwisha, hakizungumzwi tena na watu, lakini bado kinafundishwa katika shule na vyuo vingi, hasa Ulaya.

Leo hii katika nchi ya Ugiriki kuna lugha ya Kigiriki Kipya kinachoendela kuandikwa kwa herufi zilezile.

Alfabeti ya Kigiriki
Α α Alfa Β β Beta
Γ γ Gamma Δ δ Delta
Ε ε Epsilon Ζ ζ Dzeta
Η η Eta Θ θ Theta
Ι ι Iota Κ κ Kappa
Λ λ Lambda Μ μ Mi
Ν ν Ni Ξ ξ Ksi
Ο ο Omikron Π π Pi
Ρ ρ Rho Σ σ Sigma
Τ τ Tau Υ υ Ipsilon
Φ φ Phi Χ χ Khi
Ψ ψ Psi Ω ω Omega

Ulingano wa Kigiriki cha Kale na cha Kisasa

Kigiriki cha Kisasa Kigiriki cha Kale
1 Στην αρχή ήταν ο Λόγος, και ο Λόγος ήταν προς τον Θεό(ν), και Θεός ήταν ο Λόγος. 1 Ἐν ἀρχῇ ἦν ὁ Λόγος, καὶ ὁ Λόγος ἦν πρὸς τὸν Θεόν, καὶ Θεὸς ἦν ὁ Λόγος.
/stin ar'khi 'itan o 'logos ke o 'logos 'itan pros ton thi'o ke thi'os 'itan o 'logos/ /en ar'khe en o logos kaí o lógos en prós tón the'on kaí the'os en o lógos/
Kwa Kiswahili: Hapo mwanzo, kulikuwa na Neno; naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. (Injili ya Yohane, 1,1)

Viungo vya nje

Globe of letters.svg Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kigiriki kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Agano la Kale

Agano la Kale ni mkusanyo wa vitabu vya sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo inayotumiwa na waumini wa Ukristo duniani kote. Pengine mkusanyo huu unagawanywa katika makundi kadiri ya mada au mtindo: sheria, historia, ushairi na unabii, ambayo ni tofauti kiasi na kawaida ya Tanakh ya Uyahudi wa leo.

Vitabu vyote vya Agano la Kale viliandikwa kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kwa mujibu wa wanahistoria wa Biblia, vitabu vya Agano la Kale viliandikwa kati ya karne ya 11 KK na karne ya 1 KK.

Alfabeti

Alfabeti ni kiasi cha alama zinazotumiwa kuandika sauti za lugha fulani. Alama hizi hupatikana kama orodha kwa ufuatano uliokubaliwa, kwa mfano katika Kiswahili: "a, b, ch, d, dh, e, f, g, gh, h, i, j, k, kh, l, m, n, ny, ng', o, p, r, s, sh, u, t, th, v,w, y, z".

Jina la "alfabeti" hutokana na mwandiko wa Kigiriki ambamo herufi mbili za kwanza ni α "alfa" na β "beta".

Alfabeti ni mtindo wa mwandiko uliosambaa duniani kote. Kwa lugha nyingi imechukua nafasi ya miandiko ya awali.

Alfabeti huonyesha sauti si maneno kamili - hii ni tofauti na mwandiko kama Kichina wenye alama kwa ajili ya neno lote.

Alfabeti ya Kigiriki

Alfabeti ya Kigiriki ni mwandiko maalumu wa lugha ya Kigiriki. Herufi zake zilitumika pia kama tarakimu na sasa hutumiwa kimataifa kama alama za kisayansi.

Askofu mkuu

Askofu mkuu ni cheo cha askofu kiongozi anayesimamia maaskofu katika jimbo la kanisa lenye dayosisi mbalimbali.

Asili ya neno lenyewe ni Kigiriki αρχή arché (mwanzo, wa kwanza). Sehemu ya pili ni neno la Kigiriki επίσκοπος episkopos (mwangalizi) lililofikia Kiswahili kupitia umbo la Kiarabu uskuf.

Biblia

Biblia ni jina la jumla kwa ajili ya vitabu vitakatifu vya dini ya Uyahudi na hasa ya Ukristo.

Neno limetokana na lugha ya Kigiriki ambayo ndani yake βιβλία (biblia) ina maana ya "vitabu" ikiwa ni wingi wa βιβλος (biblos). Hii ni kwa sababu Biblia ni mkusanyo wa maandiko mbalimbali yaliyoweza kutungwa kwa muda wa miaka 1000 hivi.

Hivyo Biblia ni tofauti na vitabu vingine kwa sababu iliandikwa na watu mbalimbali ambao hawakuwa pamoja wala hawakuandika kwa wakati mmoja, lakini vitabu vyote vimekusanywa na kuunda kitabu kimoja cha Biblia. Inasadikiwa na Wayahudi na Wakristo kwamba "Biblia ni kitabu kilichoandikwa na watu kwa uwezo wa Mungu".

Tunaweza kutofautisha:

Biblia ya Kiebrania au Tanakh inavyotumiwa na Wayahudi. Vitabu hivyo 39 kwa Kanisa Katoliki na wengineo ni sehemu kuu ya vile 46 vinavyoitwa "Agano la Kale" (wakati Wakristo wengine, hasa Waprotestanti, wanakubali hivyo 39 tu). Ndilo sehemu ya kwanza ya

Biblia ya Kikristo inavyotumiwa na Wakristo yenye vitabu vya Agano la Kale pamoja na Agano Jipya.

Dayosisi

Dayosisi (kwa Kilatini dioecesis, kutokana na Kigiriki διοίκησις, dioikesis, yaani "utawala") ni jina linalotumika katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo (kwa mfano Walutheri na Waanglikana kumaanisha kitengo kilichopo chini ya usimamizi wa askofu katika eneo fulani.

Wakatoliki wanaoongea Kiswahili wanaiita jimbo, lakini kwa lugha nyingine wanatumia neno kama hilo bila ya kulitafsiri; kwa mfano "diocese" (Kiingereza), "diocesi" (Kiitalia) au "diocèse" (Kifaransa).

Haki

Haki ndiyo utaratibu unaotakiwa katika mafungamano.

Kwa Kigiriki inaitwa dikaiosyne, kutokana na neno asili dike yaani anayeelekeza na kwa hiyo pia mwongozo, utaratibu. Tofauti na nomos, yaani sheria inayoongoza wanyama pia, dike inahitajiwa na binadamu ili kuishi kwa utaratibu. Ni kinyume cha bie, ukatili, nguvu inayoangamiza. Dikaios (mwenye kujali haki), ni mtu anayemtendea kila mmoja haki yake. Dikaia zoe ni maisha ya kiutu yanayopingana na hybris (kiburi) na ushenzi.

Kwa Kilatini kutokana na neno jus, haki, linapatikana neno justus, mwenye kujali haki, na hatimaye justitia, iliyo adili la msingi la utu linalotufanya tumpatie mwingine anachostahili.

Maana ya haki inatofautiana Kwa kila utamaduni. Katika maana ya kwanza kabisa ambayo ilitafsiriwa na mwanafalsafa wa Ugiriki, Plato kwenye kazi yake Jamhuri. Kutokana na historia dhana mbalimbali zimegunduliwa.

Historia

Historia (kutoka Kigiriki ιστορια, historia; pia "tarehe" kutoka Kiarabu تاریخ tarih kwa maana ya "historia": pia tena "mapisi") ni somo kuhusu maisha ya binadamu na utamaduni wao wakati uliopita.

Mara nyingi neno hilo lina pia maana ya maarifa yoyote kuhusu wakati uliopita, yawe au yasiwe maarifa ya watu (kwa mfano "historia ya ulimwengu").

Historia ni hasa mfululizo wa habari za mambo yaliyotokea pamoja na sababu zake.

Binadamu anaziandika ili kuelewa maisha yake, yaani ametokea wapi, amepata mafanikio gani na matatizo gani.

Historia inatufundisha kuishi: kumbukumbu za mambo ya zamani (vita, uhuru, viongozi na mengineyo) zinatuwezesha kuendelea vizuri zaidi.

Wanahistoria wanapata maarifa yao kutoka maandishi ya zamani (hasa kwa historia andishi), kutoka fasihi simulizi na kutoka akiolojia (hasa kwa historia ya awali).

Jenasi

Jenasi (kutoka Kigiriki Γένος genos / Kilatini genus "nasaba, ukoo, familia, aina") ni ngazi katika uainishaji wa kisayansi unaopanga viumbehai (mimea, wanyama) katika vikundi kulingana na nasaba zao.

Jenasi moja huwa na spishi ndani yake. Jenasi kwa pamoja hupangwa katika familia.

Katika jina la Kisayansi la kiumbehai ni lazima kutaja jenasi. Kwa mfano paka anaitwa "Felis silvestris catus". Felis ni jina la jenasi. Jenasi huandikwa kwa herufi kubwa.

Liturujia ya Ugiriki

Liturujia ya Ugiriki, iliyoenea kutoka Konstantinopoli, sasa Istanbul (nchini Uturuki) ni liturujia ambayo lugha yake asili ni Kigiriki, lakini siku hizi inaadhimishwa katika lugha nyingine nyingi kukiwa na tofauti ndogondogo duniani kote.

Wanaoitumia hasa ni Waorthodoksi wote na baadhi ya Makanisa Katoliki ya Mashariki: hivyo ni ya pili kwa uenezi baada ya liturujia ya Roma.

Vitabu vyake vinaongoza Liturujia ya Kimungu (Ekaristi), Vipindi vya sala rasmi, Mafumbo matakatifu (Sakramenti) na sala, baraka na mazinguo mbalimbali, vilivyostawi katika Kanisa la Konstantinopoli.

Liturujia hiyo inahusika pia na namna maalumu za usanifu majengo, picha takatifu, muziki wa liturujia, mavazi na mapokeo zilizostawi vilevile karne hata karne kila ilikotumika.

Kwa kawaida mkusanyiko wa waamini huwa wamesimama muda wote wa ibada, na ukuta wa picha takatifu unaoitwa iconostasis unawatenganisha na patakatifu anapohudumia askofu au padri akisaidiwa na shemasi.

Ushiriki wa walei unajitokeza katika kusujudu mara nyingi na kuitikia sala na nyimbo.

Katika liturujia hiyo Biblia inatumika sana katika masomo na katika matini mengine vilevile.

Taratibu za saumu ni kali kuliko zile za Ukristo wa Magharibi na zinafuatwa katika vipindi vinne kwa mwaka: Kwaresima Kuu, Kwaresima ya Noeli, Mfungo wa Mitume na Mfungo wa Kulala kwa Bikira Maria. Pamoja na hayo, Jumatano na Ijumaa nyingi ni za kufunga chakula. Monasteri nyingi zina mfungo hata Jumatatu zote.

Makanisa Katoliki ya Mashariki

Makanisa Katoliki ya Mashariki ni madhehebu 23 ya Ukristo ambayo yanafuata mapokeo mbalimbali ya Mashariki katika ushirika kamili na Askofu wa Roma (Papa), hivyo pia na Kanisa Katoliki lote duniani.

Mapokeo hayo ni hasa yale ya Aleksandria (Misri), Antiokia (kihistoria jiji la Siria, leo nchini Uturuki), Konstantinopoli (kihistoria jiji la Ugiriki, leo nchini Uturuki), Armenia na Wakaldayo (kihistoria Mesopotamia, leo Iraq).

Baadhi ya mapokeo hayo yamezaa matawi, kama ya Misri yale ya Ethiopia na Eritrea.

Pamoja na hayo, kama Makanisa ya Waorthodoksi, hayo pia yanaambatana na utamaduni wa taifa, na kuyafanya yagawanyike kiutawala hata kama teolojia, liturujia n.k. zinaendelea kuwa zilezile kadiri ya mapokeo.

Kwa jumla yanakubali kuwa mapadre watu waliooa lakini hawana maaskofu waliooa.

Mita

Mita (pia: meta) ni kipimo cha urefu ambacho kimekuwa kipimo sanifu cha kimataifa.

Neno limetokana na Kigiriki μέτρον/métron (kipimo, pia chombo cha kupimia), kwa kupitia Kiingereza "metre, meter".

Kutokana na maana hiyo "mita" inataja pia mitambo ya kupima maji, umeme na kadhalika. Hapo matumizi ya Kiswahili yanafanana na ya Kiingereza "metre".

Mkoa wa İzmir

İzmir ni jina la kutaja moja kati ya Mikoa ya Uturuki uliopo mjini magharibi mwa Anatolia kwenye pwani ya Bahari ya Aegean. Mji mkuu wa mkoani hapa ni Izmir. Mji huu ulianzishwa na Wagiriki Smyrna (Kigiriki: Σμύρνη) kunako karne ya 11 KK. Kwa upande magharibi umezungukwa na Bahari ya Aegean, na imefungamana kabisa na Ghuba ya İzmir. Mkoa umechukua eneo la kilomita za mraba zipatazo 11,973. Takriban watu 3,769,000 wanaishi mjini hapa (makisio ya 2007). Idadi ya wakazi wa hapa ilikuwa 3,370,866 kunako mwaka wa 2000. Mikoa ya jirani na mkoa ni pamoja na Balıkesir katika upande wa kaskazini, Manisa kwa upande wa mashariki, na Aydın kwa upande wa kusini.

Muziki

Muziki ni aina ya sanaa inayotumia sauti mbalimbali: za kibinadamu na za ala za muziki, ama kwa pamoja au kila moja pekee.

Asili ya neno iko katika lugha ya Kigiriki ambamo huitwa μουσική (mousikee).

Baadhi ya sifa za muziki ni uzito wa sauti (pitch) na wizani au mahadhi (rhythm).

Aina ya muziki inayopatikana kote duniani ni nyimbo ambazo ni maneno yanayotolewa kwa sauti na mahadhi fulani mara nyingi pamoja na ala za muziki. Kwa wanaorekodi sauti, wao huenda kwa studio kurekodi na huchukuliwa kwa kinasasauti kilichoambatanishwa na tarakilishi na kudhibitiwa na kompresa.

Neema

Neema ni jambo lolote jema ambalo binadamu anapata katika maisha yake.

Neno hilo kwa Kiswahili ni pana, lenye maana mbalimbali, kama vile mema ya kiroho na ya kiuchumi, lakini zote zinaelekeza kumfikiria Mungu kama asili yake kuu. Ni huruma ya Mungu kwa wanadamu inayoambatana na baraka.

Teolojia katika dini mbalimbali inatumia neno hili kadiri ya imani yake.

Kwa namna ya pekee neno linatiwa mkazo katika Ukristo unaosisitiza kwamba mambo yote ni neema (kwa Kigiriki: χάρις, kharis; kwa Kilatini: gratia, yaani deso, kitu cha bure).

Hata hivyo madhehebu yake yanatofautiana sana katika kutafsiri tamko hilo.

Shirika la Kimataifa la Usanifishaji

Shirika la Kimataifa la Usanifishaji (kwa kifupi ISO) ni shirika lenye wajibu wa kuandaa na kutekeleza vipimo vya pamoja kwa sehemu mbalimbali za teknolojia na uchumi duniani. Jina limechaguliwa kutokana na neno la Kigiriki ίσος (isos) linalomaanisha "sawa".

Kuna mashirika mawili yanayoshirikiana nalo ambayo ni Kamati ya Kimataifa kwa Teknolojia ya Umeme na Umoja wa Kimataifa wa Vyombo vya Mawasiliano yanayoshughulika teknolojia za kuhusiana na fani zao na zote kwa pamoja ni Umoja wa Usanifishaji wa Dunia.

ISO iliundwa mwaka 1947 kama ushirikiano wa nchi 25 zilizoamua kuunganisha jitihadi zao za usafinishaji. Makao makuu yako Geneva (Uswisi). Hadi leo kuna nchi wanachama 163 kati ya mataifa 203 za dunia.

Vipimo vinavyokubaliwa hutolewa namba inayoanza kwa herufi ISO kwa mfano ISO 8601 kuhusu namna ya kuandika wakati na tarehe, ISO 4217 kuhusu kutaja hela za nchi za dunia au ISO 668 inayotawala vipimo vya kontena zinazokubaliwa katika biashara ya kimataifa.

Tarakimu

Tarakimu (kutoka Kiarabu رقم raqm) au numerali (kutoka Kilatini numerus, kupitia Kiingereza numeral) ni alama za kimaandishi zinazotumiwa kuandika namba.

Teolojia

Teolojia, pia theolojia na thiolojia (kutoka maneno ya Kigiriki θέος, theos, "Mungu" + λογία, logia, "usemi") ni elimu juu ya Mungu hasa katika Ukristo. Hiyo haitenganiki na utendaji wake wa nje, yaani uhusiano wake na viumbe vyote.

Jina lingine la fani hiyo lenye asili ya Kiarabu ni Tauhidi. Hilo linatumiwa zaidi na Waislamu. Kwa Kiswahili limetungwa pia jina "Taalimungu".

Basi, ikitajwa kwa jina la mkopo kutoka Kigiriki, fani hiyo inachunguza hasa imani ya Kikristo kadiri ya Ufunuo wa Mungu uliokamilika katika Yesu Kristo na Mitume wake.

Kwa sababu hiyo inategemea hasa Maandiko Matakatifu ya Biblia, lakini pia, kadiri ya madhehebu husika, Mapokeo ya Mitume yasiyoandikwa pamoja na mamlaka hai ya Kristo waliyonayo maaskofu (Ualimu wa Kanisa).

Teolojia hufundishwa katika vyuo na katika nchi mbalimbali; iko pia kama idara ya Chuo Kikuu. Idara hizi mara nyingi zinatenganishwa kimadhehebu. Mtu aliyepita mafundisho ya chuo huitwa mwanateolojia.

Ugiriki

Ugiriki (pia: Uyunani; kwa Kigiriki: Ελλάδα, Ellada, au Ελλάς, Ellas) ni nchi ya Ulaya Kusini-Mashariki katika kusini ya rasi ya Balkani.

Imepakana na Albania, Masedonia Kaskazini, Bulgaria na Uturuki.

Upande wa kusini-magharibi na kusini-mashariki kuna pwani ndefu kwenye Bahari ya Mediteranea.

Baharini huko kuna visiwa vingi sana ambavyo ni sehemu za Ugiriki.

Ugiriki ni nchi yenye historia ndefu na maarufu sana, hata inaitwa "nchi mama ya Ulaya".

Lugha ya Kigiriki inaendelea kuandikwa kwa Alfabeti ya Kigiriki inaotumiwa tangu miaka 3000 iliyopita, lakini lugha yenyewe imebadilika. Wagiriki wa leo hawaelewi tena Kigiriki cha Kale moja kwa moja.

Wakazi wengi wanafuata dini ya Ukristo, hasa katika Kanisa la Kiorthodoksi la Kigiriki (97%). 1.3% ni Waislamu.

Ugiriki ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya tangu 1981.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.