Kiebrania

Lugha ya Kiebrania (עברית ‘Ivrit, Loudspeaker.png matamshi ya kisasa ?) ni moja ya lugha za kisemiti na moja kati ya lugha mbili za kitaifa nchini Israel (pamoja na Kiarabu). Ni kati ya lugha za kale zaidi duniani.

Kiebrania kwa kawaida huandikwa kwa herufi za Kiebrania. Mwandiko huu ni wa konsonanti hasa, kwa kuwa mara nyingi vokali haziandikwi kutokana mfumo wa lugha yenyewe.

Kiebrania ni lugha iliyotumika kuandikia Torati na sehemu kubwa ya maandiko mengine ya Biblia ya Kiebrania. Sehemu hiyo ya Kiebrania pamoja na sehemu ndogo ya Kiaramu huitwa "Tanakh" katika mapokeo ya Kiyahudi na imo katika Agano la Kale ya Biblia ya Kikristo.

Israel in Hebrew
"jisrael" ni neno "Israel" kwa lugha ya Kiebrania na kwa mwandiko wa Kiebrania

Lugha za Kisemiti

Lugha ya Kiebrania pamoja na zile za Kiarabu, Kiaramu na Kiamhari (Ethiopia) zinatokana na asili moja ya lugha ya Kisemiti. Kuna lugha nyingi ambazo zinatokana na asili hiyohiyo kama Kiashuru, Kifoinike, Kikaldayo na kadhalika.

Mwandiko wa Kiebrania

Makala Kuu: Mwandiko wa Kiebrania

Mwandiko wa lugha hiyo hufanywa kwa mwandiko wa pekee unaojulikana tangu miaka 3,000. Mwandiko huu ni wa konsonanti hasa, kwa kuwa mara nyingi vokali haziandikwi. Tabia hii ni sawa na alfabeti nyingine za Kisemiti kama Kiaramu au Kiarabu.

Mfano: Jina la Abrahamu huandikwa "אַבְרָהָ֛ם" ambazo ni herufi "aBRHM" pekee; Alef ambayo ni herufi la kwanza tena si "a" kwa hakika. Vokali zinaweza kuonyeshwa kwa nukta na mistari chini ya herufi lakini mara nyingi haziandikwi.

Alef Bet/Vet Gimel Dalet He Waw Zayin Khet Tet Yod Kaf/Khaf
א ב ג ד ה ו ז ח ט י כ
ך
Lamed Mem Nun Samekh Ayin Pe/Fe Tsadeh Qof Resh Shin/Sin Taw
ל מ נ ס ע פ צ ק ר ש ת
ם ן ף ץ

Historia

Kiebrania kilikuwa lugha ya Israeli ya Kale wakati wa Biblia kuanza kuandikwa. Baada ya Uhamisho wa Babeli Wayahudi walianza kutumia Kiaramu, na polepole Kiebrania hakikuzungumzwa tena, lakini kilifundishwa kama lugha ya kidini. Wayahudi wa kawaida walikitumia katika ibada na wataalamu waliandika vitabu kwa lugha hiyo.

Katika karne ya 20 Wayahudi wa Ulaya waliamua kukifufua kama lugha hai. Kimekuwa lugha ya nchi mpya ya Israel tangu 1948. Watu waliohamia Israel kutoka mahali pengi duniani walijifunza Kiebrania na watoto wao wameishika kama lugha yao ya kawaida.

Viungo vya nje

Agano la Kale

Agano la Kale ni mkusanyo wa vitabu vya sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo inayotumiwa na waumini wa Ukristo duniani kote. Pengine mkusanyo huu unagawanywa katika makundi kadiri ya mada au mtindo: sheria, historia, ushairi na unabii, ambayo ni tofauti kiasi na kawaida ya Tanakh ya Uyahudi wa leo.

Vitabu vyote vya Agano la Kale viliandikwa kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo. Kwa mujibu wa wanahistoria wa Biblia, vitabu vya Agano la Kale viliandikwa kati ya karne ya 11 KK na karne ya 1 KK.

Alfabeti

Alfabeti ni kiasi cha alama zinazotumiwa kuandika sauti za lugha fulani. Alama hizi hupatikana kama orodha kwa ufuatano uliokubaliwa, kwa mfano katika Kiswahili: "a, b, ch, d, dh, e, f, g, gh, h, i, j, k, kh, l, m, n, ny, ng', o, p, r, s, sh, u, t, th, v,w, y, z".

Jina la "alfabeti" hutokana na mwandiko wa Kigiriki ambamo herufi mbili za kwanza ni α "alfa" na β "beta".

Alfabeti ni mtindo wa mwandiko uliosambaa duniani kote. Kwa lugha nyingi imechukua nafasi ya miandiko ya awali.

Alfabeti huonyesha sauti si maneno kamili - hii ni tofauti na mwandiko kama Kichina wenye alama kwa ajili ya neno lote.

Bahari ya Mediteranea

Bahari ya Mediteranea (pia: Bahari ya Kati) ni bahari ya pembeni ya Atlantiki kati ya mabara ya Afrika, Ulaya na Asia ya Magharibi. Eneo lake ni takriban milioni 2,5 km². Kina chake kirefu ni 5,267 m. Ina kanda ya hali ya hewa ya pekee pamoja na mimea na wanyama.

Neno "Mediteranea" limetokana na lugha ya Kilatini likiunganisha maneno ya "medium" (inamaanisha "kati ya, katikati") na "terra" (inamaanisha "bara"). Kwa hiyo neno lenyewe linamaanisha "Bahari katikati ya bara".

Katika lugha ya Biblia Kiebrania iliitwa "Bahari ya Magharibi" au "Bahari Kuu"; Waroma wa Kale waliotwala nchi zote zinazopakana na Bahari ya Mediteranea waliita "mare nostrum" yaani "bahari yetu". Waarabu na Waturuki wanaiita "Bahari Nyeupe" (Kitur. Akdeniz au Kiarab. البحر الأبيض al-baHr-al-abyaD)

Biblia

Biblia ni jina la jumla kwa ajili ya vitabu vitakatifu vya dini ya Uyahudi na hasa ya Ukristo.

Neno limetokana na lugha ya Kigiriki ambayo ndani yake βιβλία (biblia) ina maana ya "vitabu" ikiwa ni wingi wa βιβλος (biblos). Hii ni kwa sababu Biblia ni mkusanyo wa maandiko mbalimbali yaliyoweza kutungwa kwa muda wa miaka 1000 hivi.

Hivyo Biblia ni tofauti na vitabu vingine kwa sababu iliandikwa na watu mbalimbali ambao hawakuwa pamoja wala hawakuandika kwa wakati mmoja, lakini vitabu vyote vimekusanywa na kuunda kitabu kimoja cha Biblia. Inasadikiwa na Wayahudi na Wakristo kwamba "Biblia ni kitabu kilichoandikwa na watu kwa uwezo wa Mungu".

Tunaweza kutofautisha:

Biblia ya Kiebrania au Tanakh inavyotumiwa na Wayahudi. Vitabu hivyo 39 kwa Kanisa Katoliki na wengineo ni sehemu kuu ya vile 46 vinavyoitwa "Agano la Kale" (wakati Wakristo wengine, hasa Waprotestanti, wanakubali hivyo 39 tu). Ndilo sehemu ya kwanza ya

Biblia ya Kikristo inavyotumiwa na Wakristo yenye vitabu vya Agano la Kale pamoja na Agano Jipya.

Biblia ya Kiebrania

Biblia ya Kiebrania ni namna mojawapo ya kutaja vitabu vitakatifu vya Uyahudi vinavyoitwa na Wayahudi wenyewe "Tanakh". Ndivyo vinavyounda pia sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo na kuitwa na Wakristo "Agano la Kale" (vikiwa pamoja na Deuterokanoni au vikiwa peke yake).

Vitabu hivyo, vilivyoandikwa kwa Kiebrania na sehemu ndogo kwa Kiaramu, vinaheshimiwa pia na Wakristo wakiamini ya kwamba ufunuo wa vitabu hivyo ulikuwa hatua ya kwanza iliyokamilishwa baadaye na hatua ya pili au "Agano Jipya" kwa ujio wa Yesu Kristo.

Kuna madhehebu na wataalamu wanaopendelea kuviita vitabu hivyo kwa jina la Biblia ya Kiebrania ili wasisitize usawa wa vitabu vilivyofunuliwa au wasionekane wanavikosea heshima vitabu ambavyo kwa Wayahudi si jambo la "kale".

Hivyo kichwa cha Kilatini "Biblia Hebraica" limekuwa jina la kawaida kwa matoleo ya kitaalamu ya maandiko haya.

Hata hivyo majina "Agano la Kale" na "Agano Jipya" yanapatikana katika Biblia yenyewe (taz. hasa Eb 8).

Biblia ya Kikristo

Biblia ya Kikristo ni mkusanyo wa maandiko matakatifu ya Ukristo. Maandiko hayo mbalimbali yanaitwa tangu zamani sana "vitabu" tu, inavyomaanishwa na neno la Kigiriki βιβλια, "biblia" ambalo ni wingi wa neno "biblos" yaani "kitabu".

Hutofautishwa na Tanakh ambayo ndiyo maandiko matakatifu ya dini ya Uyahudi na ambayo pengine inatajwa kwa jina lilelile la "Biblia", hasa katika matoleo ya Biblia ya Kiebrania. Vitabu vyake vimo katika sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo kwa jina la "Agano la Kale".

Biblia ya Kikristo hugawiwa sehemu mbili ambayo ni Agano la Kale na Agano Jipya. Agano la Kale lina maandiko yaliyoandikwa kabla ya Yesu Kristo na vitabu vya Agano Jipya viliandikwa baada yake.

Israel

Kwa maana mbalimbali za jina Israeli katika Biblia tazama Israeli (maana)

Israel (kwa Kiebrania: מדינת ישראל - Medinat Yisra'el; kwa Kiarabu: دَوْلَةْ إِسْرَائِيل - dawlat Isrā'īl) ni nchi ya Mashariki ya Kati kwenye mwambao wa mashariki wa Mediteranea.

Imepakana na Lebanon, Syria, Yordani, Misri na maeneo yaliyo chini ya mamlaka ya serikali ya Palestina.

Kigiriki

Kigiriki (pia: Kiyunani) ni lugha ya Kihindi-Kiulaya inayotumiwa hasa nchini Ugiriki. Maandishi yake yamejulikana tangu miaka 3500 iliyopita. Hakuna lugha nyingine duniani inayozungumzwa hadi leo yenye historia ndefu kuliko hii, isipokuwa Kichina.

Kigiriki ni muhimu sana kwa utamaduni wa kisasa kwa sababu ya kutoa michango mingi kwa lugha ya sayansi, teknolojia na utamaduni. Fikra nyingi muhimu zilionekana mara ya kwanza kwa Kigiriki na falsafa iliyojadiliwa na kuandikwa kwa lugha hii. Istilahi nyingi za kisayansi zimetoka katika Kigiriki.

Alfabeti ya Kigiriki ilikuwa msingi wa alfabeti nyingine mbili, za Kilatini na Kikirili, pia kwa miandiko ya abijadi kama herufi za Kiarabu au za Kiebrania. Kiswahili huandikwa leo kwa herufi za Kilatini.

Kati ya maandiko muhimu ya Kigiriki ni yale ya wanafalsafa kama Plato na Aristoteles na pia baadhi ya maandiko ya Biblia ya Kikristo (Agano Jipya pamoja na Deuterokanoni), mbali ya tafsiri ya kwanza ya Biblia ya Kiebrania maarufu kwa jina la Septuaginta (karne ya 2 KK).

Kati ya karne ya 3 KK hadi karne ya 6 BK Kigiriki kilikuwa lugha ya kimataifa katika eneo kubwa la kandokando ya bahari ya Mediteranea pamoja na Mashariki ya Kati.

Lugha imeendelea kubadilika kisarufi, kimatamshi na pia kimsamiati. Hivyo Kigiriki cha kale kimekwisha, hakizungumzwi tena na watu, lakini bado kinafundishwa katika shule na vyuo vingi, hasa Ulaya.

Leo hii katika nchi ya Ugiriki kuna lugha ya Kigiriki Kipya kinachoendela kuandikwa kwa herufi zilezile.

Kitabu cha Esta

Kitabu cha Esta (jina lake huandikwa pia Ester na "Esther") ni kitabu cha Biblia ya Kiebrania, na hivyo pia cha Agano la Kale, ambalo ni sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo. Kiliandikwa kwanza kwa Kiebrania.

Tafsiri ya kitabu cha Esta inavyopatikana katika Septuaginta imeongezewa sana; nyongeza hizo za Kigiriki zinahesabiwa na Kanisa Katoliki na wengineo kuwa sehemu za kitabu yenye uvuvio wa Roho Mtakatifu ingawa si sehemu za hadithi asili. Ni katika nyongeza hizo tu kwamba Mungu anatajwa na mtazamo wa imani unajitokeza.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Kitabu cha Nahumu

Kitabu cha Nahumu (kwa Kiebrania נחום, Nahum) ni kimojawapo kati ya vitabu 12 vya gombo la Manabii wadogo katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na kwa hiyo pia katika Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.

Lugha za Kiafrika-Kiasia

Lugha za Kiafrika-Kiasia ni familia ya lugha barani Afrika na Asia. Katika familia hiyo kuna lugha zaidi ya 300 zenye wasemaji milioni 350 kati ya Afrika ya Kaskazini na Asia ya Magharibi, hasa Kiarabu, lakini pia Kihausa, Kioromo, Kiamhara, Kisomali, Kiebrania n.k.

Maombolezo (Biblia)

Kitabu cha Maombolezo (kwa Kiebrania איכה, eikha) ni kama nyongeza ya kitabu cha nabii Yeremia katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na hivyo pia katika Agano la Kale iliyo sehemu ya kwanza ya Biblia ya Kikristo.

Kichwa chake kinadokeza kwamba ni mashairi matano ya uchungu kuhusu maangamizi ya Yerusalemu (587 K.K.) na uhamisho wa Babeli uliofuata kwa Wayahudi wengi.

La kwanza, la pili na la nne yanazingatia utaratibu wa kwamba kila mstari unaanza na herufi tofauti kufuatana na alfabeti ya Kiebrania yenye herufi 22.

Katika mashairi hayo matano inaonekana toba halisi iliyotokana na tukio hilo lililotazamwa kuwa adhabu ya Mungu kwa dhambi za taifa lake.

Hatujui yametungwa na nani.

Kama vitabu vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Mlolongo wa Kitume

Mlolongo wa Kitume (kwa Kiebrania האפיפיור הירושה, kwa Kigiriki Αποστολική διαδοχή) ni jambo linalodaiwa na imani ya baadhi ya madhehebu ya Ukristo, ya kwamba ni lazima viongozi wa Kanisa washiriki mamlaka ya Mitume wa Yesu katika mlolongo usiokatika wa kuwekewa mikono na maaskofu katika kuwapatia daraja takatifu.

Imani hiyo inatiwa maanani hasa na Kanisa Katoliki, Waorthodoksi, Waorthodoksi wa Mashariki, lakini pia Waanglikana na wengineo.

Kwao, maaskofu wa leo ni waandamizi wa wale wa jana na juzi hata kurudia kwa wale waliowekewa mikono na mitume wenyewe katika karne ya 1.

Mlolongo huo unahakikisha uhalali wa mamlaka yao katika kufundisha, kutakasa na kuongoza.

Kwa madhehebu mbalimbali ya Uprotestanti, suala la mikono si la lazima, kwani kwao ni muhimu zaidi kuendeleza mafundisho ya mitume.

Msalaba wa Yesu

Msalaba wa Yesu ni msalaba ule ambao Yesu Kristo alisulubiwa juu yake huko Yerusalemu kwa amri ya Ponsyo Pilato siku ya Ijumaa, labda tarehe 7 Aprili 30 BK.

Tukio hilo, pamoja na ufufuko wa Yesu unaosadikiwa na Ukristo kutokea siku ya tatu (Jumapili ya Pasaka), ndiyo kiini cha imani ya dini hiyo mpya iliyotokana na ile ya Uyahudi.

Kwa Wakristo fumbo hilo la Pasaka ndilo kilele cha historia ya wokovu inayotangazwa na Biblia ya Kikristo.

Fumbo hilo lilisababisha kazi nyingi za sanaa ya Kikristo, hasa uchoraji na uchongaji.

Nabii

Neno nabii (kwa Kiebrania נביא nevì, kwa wingi נְבִיאִים nevi'ìm, kwa Kiarabu نبي) linatumika kumtajia binadamu anayesema kwa niaba ya Mungu, hasa kwa kusudi la kuelekeza wenzake wafuate imani na maadili sahihi.

Katika lugha nyingi, mtu huyo anaitwa kwa jina linalotokana na neno la Kigiriki προφήτης [prophētēs], maana yake "anayesema mbele", yaani hadharani (mbele ya wasikilizaji), au kabla ya (jambo kutokea).

Watu wa namna hiyo wanapatikana katika dini nyingi, hususan katika Uyahudi, Ukristo na Uislamu.

Katika matumizi ya kawaida, neno hilo linatumika hasa kwa mtu ambaye anatabiri jambo, bila ya kujali asili ya maarifa yake.

Tanakh

Tanakh (תנ״ך) ni jina la Kiebrania la Biblia ya Kiyahudi.

Tanakh ni kifupi kinachounganisha herufi tatu "T" - "N" - "Kh" ambazo ni mianzo ya maneno matatu ya Kiebrania yanayotaja sehemu tatu ndani ya Biblia ya Kiebrania.

1. Torah (תורה) ni Torati au vitabu vitano vya kwanza vinavyoitwa pia "vitabu vya Musa". Mara nyingi vyaitwa pia "sheria" katika imani ya Uyahudi. Hivi ni vitabu vinavyoitwa ama Kitabu cha kwanza, cha pili, cha tatu cha Musa au kwa majina yafuatayo:

Mwanzo, Kutoka, Mambo ya Walawi, Hesabu na Kumbukumbu la Torati.

Majina ya Kiebrania ya vitabu hivi ni maneno ya kwanza ya Kiebrania ya kila kitabu: Bereshit (בְּרֵאשִית) yaani mwanzo (Hapo mwanzo..); Shemot (שְמוֹת) yaani majina (Basi majina ya wana wa Israeli...); Wayikra (וַיִּקְרָא) yaani "akaita" (Bwana akamwita Musa...); Bemidbar (בְּמִּדְבַּר) yaani "porini, nyikani" (Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai = nyika ya Sinai...); Devarim (דְּבָרִים) yaani "maneno" (Haya ndiyo maneno...)2. Nevi'im (נביאים) ni manabii yaani maandiko ya maneno na matendo ya manabii katika Uyahudi. Humo huhesabiwa vitabu kama

Yoshua, Waamuzi, Samweli 1, Samweli 2, Wafalme 1 na Wafalme 2

Isaya, Yeremia, Ezekieli na kitabu cha "manabii wadogo" 12 (Hosea, Yoeli, Amosi, Obadia, Yona, Mika, Nahumu, Habakuki, Sefania, Hagai, Zekaria, Malaki)3. Ketuvim (כתובים) ni "maandiko" (Kiebrania "ketuv" ni sawa na Kiarabu/ Kiswahili "kitab/kitabu"). Vitabu hivi hugawanywa katika kundi za

vitabu vya kihistoria kama vile Ezra, Nehemiah na Mambo ya Nyakati .

vitabu vya hekima kama vile Ayubu, Mhubiri na Mithali.

vitabu vya kishairi kama vile Zaburi, Maombolezo na Wimbo Ulio Bora.

vitabu vingine kama vile Ruthu, Estha na Danieli.Mgawanyo huo wa vitabu ni tofauti kiasi na namna ya kuvipanga katika Biblia ya Kikristo vinamopatikana katika sehemu ya kwanza ambayo inaitwa Agano la Kale na kufuatwa na Agano Jipya lililoandikwa baada ya Yesu ambaye Wakristo wanaamini ndiye Masiya aliyetabiriwa tangu kale.

Hasa Wakristo wanawauliza kaka zao Wayahudi: imekuwaje ufunuo wa Mungu kwao ulisimama tangu miaka zaidi ya 2000 ingawa wao wanamsubiri bado Masiya afike? Je, historia ya wokovu imekatika?

Wikipedia ya Kiebrania

Wikipedia ya Kiebrania (Kiebrania: ויקיפדיה: האנציקלופדיה החופשית; inamtamkwa Wikipedia: HaEntziklopedia HaHofshit, wakati Wikipedia inatamkwa na baadhi yao Vikipedia; wikiˈpedia haʔentsikloˈpedia haχofˈʃit) ni toleo la kamusi elezo ya Wikipedia kwa lugha ya Kiebrania. Toleo hili lilianzishwa mnamo mwezi wa Julai katika mwaka wa 2003 na kwa tar. 11 Aprili ya mwaka wa 2009, imefikisha zaidi ya makala 90,000.

Wimbo Ulio Bora

Wimbo Ulio Bora (kwa Kiebrania שיר השירים, Shir ha-Shirim), ni kitabu kimojawapo cha Tanakh (Biblia ya Kiebrania) na hivyo pia cha Agano la Kale katika Biblia ya Kikristo.

Kama vitabu vingine vyote vya Biblia, hiki pia kinatakiwa kisomwe katika mfululizo wa historia ya wokovu ili kukielewa kadiri ya maendeleo ya ufunuo wa Mungu kwa binadamu.

Yerusalemu

Yerusalemu (mara kwa mara pia Kudisi) (kwa Kiebrania ירושלים, Yerushalayim, kwa Kiarabu: القدس, al-Quds) ni mji wa Mashariki ya Kati wenye pande mbili. Kwa upande mmoja ni mji mkuu wa Israel. Kwa upande mwingine Yerusalemu ya mashariki inatazamiwa kuwa mji mkuu wa Palestina, ingawa imetawaliwa na Israel pia tangu 1967. Israel imetangaza tangu mwaka 1980 Yerusalemu yote kuwa mji wake mkuu wa milele, lakini nchi nyingi za dunia hazikubali azimio hilo, hivyo balozi za nchi za kigeni katika Israel ziko nje ya Yerusalemu.

Yerusalemu ina historia ndefu sana.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.