Kabichi

Kabichi (pia kabeji kutoka Kiingereza "cabbage") ni mboga yenye umbo la mviringo mkubwa na rangi ya kijani, nyekundu (zambarau), au nyeupe inayopandwa kwa msimu.

Kabichi inaweza kuliwa baada ya kupikwa au ikiwa mbichi na ina manufaa mengi kwa afya. Kabichi ina thamani ya juu upande wxa lishe.

Kichwa cha kabichi kwa ujumla huwa na kilo 0.5 hadi 4, na inaweza kuwa kijani, zambarau au nyeupe. Hadi mwaka 2012, kabichi nzito zaidi ilikuwa na kilo 62.71.

Kabichi inayoliwa na binadamu asili yake ni kabichi mwitu. Kabichi ilianza kupandwa huko Ulaya kabla ya mwaka 1000 KK. Katika enzi za zama za Kati, kabichi ilikuwa sehemu kubwa ya vyakula vya Ulaya.

Kwa kawaida, vichwa vya kabichi huvunwa mwaka wa kwanza wa mzunguko wa maisha ya mmea huo, lakini mimea inayotengwa kwa ajili ya mbegu inaruhusiwa kukua mwaka wa pili.

Kabichi huathiriwa na upungufu wa virutubisho kadhaa, pamoja na kuliwa na wadudu wengi, na kupatwa na magonjwa ya bakteria na ya vimelea.

Chou 1
Aina ya kabichi.

Viungo vya njə

Greentree.jpg Makala hii kuhusu mmea fulani bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Kabichi kama uainishaji wake wa kibiolojia, uenezi au matumizi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Chainizi

Chainizi (yaani "ya China", kutoka Kiingereza "Chinese leaf" au "Chinese cabbage"; jina la kisayansi: "Brassica rapa") ni aina ya mboga ya majani jamii ya kabichi za Ulaya. Kutoka China, ilipoanza kulimwa zamani sana, imeenea duniani kote.

Inatupatia afya katika miili yetu, hasa kwa sababu ina wingi wa vitamini A na C.

Mboga ya chainizi wakati wa kupikwa huwekwa vitu vifuatavyo: nyanya, kitunguu, karoti na pilipili hoho; hivyo ni vitu ambavyo huwekwa kwenye mboga ya chainizi.

Kachumbari

Kachumbari (kutoka neno la Kihindi cachumber) ni mchanganyiko wa viungo kama pilipili, chumvi na mboga na matunda mbalimbali kama nyanya, vitunguu, kabichi, matango, nanasi, parachichi n.k.

Mara nyingi hutumika pamoja na pilau, wali, nyama choma n.k. ili kuongeza ladha ya chakula.

Kachumbari ni maarufu sana katika Nchi za Maziwa Makuu.

Katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo huitwa Kachumbari.

Nchini Malawi huitwa 'Sumu' au 'Shum' au saladi ya nyanya na vitunguu.

Kidukari

Vidukari, vidukali au wadudu-mafuta ni wadudu wadogo wa familia Aphididae katika oda Hemiptera ya nusungeli Pterygota (wenye mabawa). Aphididae ni familia pekee ya familia ya juu Aphidoidea iliyopo hadi sasa; familia nyingine zimekwisha zote. Vidukari ni miongoni mwa wadudu wasumbufu sana katika kilimo na katika bustani na juu ya mimea nyumbani, kwa sababu wanafyunza utomvu wa mimea, ule wa floemi hasa lakini mara kwa mara ule wa ksilemi pia. Utomvu wa floemi una ukolezi mkubwa wa sukari na ukolezi mdogo wa asidi-amino. Ili kupata asidi-amino za kutosha, lazima kidukari afyunze utomvu mwingi na kwa sababu ya hii anapata sukari zaidi ya kiasi anachohitaji. Kiasi cha sukari kilichozidi kinatolewa kama mana (kitone cha shira chenye ukolezi mkubwa sana wa sukari: honeydew kwa Kiing.). Sisimizi wanapenda mana sana lakini hawawezi kunywa yote. Kwa hivyo mana nyingi inaanguka kwenye majani na hapa kuvu nyeusi inaanza kukua juu yake. Kuvu hii inazuia majani yasifanye usanidimwanga na mmea unanywea. Kwa bahati nzuri wakulima wana wadudu rafiki ambao hula vidukari kama wadudu-kibibi (lava na wadudu wapevu), wadudu mabawa-vena (lava na wapevu), nzi-wangamaji (lava tu), nyigu wa kidusia (lava tu), buibui-kaa n.k. Pia kuna kuvu viuawadudu (entomopathogenic fungi) inayoambukiza wadudu hawa, kama Metarhizium anisopliae, Beauveria bassiana, Isaria fumosorosea na Lecanicillium longisporum.

Vidukari ni wadudu wadogo. Wapevu wa takriban spishi zote wana urefu wa mm 1-5, lakini spishi nyingine zinaweza kufika mm 10. Kiwiliwili cha vidukari kina umbo wa pea mara nyingi au kimerefuka kidogo. Kiunzi-nje ni chororo lakini kimepakiwa nta ya kuhifadhi mara nyingi. Nta hii hutolewa kutoka mirija miwili nyuma kwenye fumbatio. Vipande vya mdomo vimeungana katika mrija pia na mrija huu hutumika ili kufyunza utomvu. Wakati wa majira mazuri vidukari hawana mabawa lakini wakati majira yanakuwa mabaya au ubora wa chakula unaanza kuwa mbaya, vidukari wenye mabawa huzaliwa ambao huhamia mimea ingine.

Jinsia ya vidukari ni ya kike kwa kawaida. Kwa hivyo mayai ya majike hukua bila kurutubishwa. Vidukari wengi zaidi huzaa lava waliotoka kwa mayai ndani ya ovarioli za mama. Lava wanafanana na mamao isipokuwa ukubwa wake. Kwa kawaida lava huambua mara nne kabla ya kuwa wapevu. Spishi nyingi huzaa madume wakati majira yanakuwa mabaya. Baada ya kupandana majike huyataga mayai ambayo yanapumzika mpaka majira mazuri.

Mawali

Mawali au mau (Moringa stenopetala, kutoka Kisomali mawali na mau) ni mti wa jenasi pekee, Moringa, ya familia Moringaceae. Asili ya mti huu ni Afrika ya Mashariki. Hupandwa katika mashamba kwa tungazi huko Konso, Uhabeshi, na hutumika kwa chakula cha watu, kupatia mimea mingine ya mazao kivuli na mitishamba.

Mdudu Mabawa-vigamba

Wadudu mabawa-vigamba ni wadudu wadogo hadi wakubwa wa oda Lepidoptera katika nusungeli Pterygota (wenye mabawa). Jina ni tafsiri ya jina la kisayansi. Wadudu hawa wanajulikana kama vipepeo na nondo.

Wadudu hawa wana mabawa kama viwambo, isipokuwa spishi kadhaa ambazo zina mabawa yaliyopunguka au hazina mabawa kabisa. Kinyume na wadudu mabawa-viwambo kwa kawaida mabawa yao yamefunikwa kwa vigamba ambavyo kweli ni manyoya yaliyofanyika kuwa bapa. Lakini mabawa ya spishi kadhaa yana sehemu bila vigamba zilizo nyangavu kwa hivyo (k.m. Nondo mkia-mshale mwangavu).

Sehemu za kinywa za spishi nyingi zimetoholewa kuwa mrija mrefu sana unaoitwa ulimi au proboski. Mrija huo hutumiwa kufyonza mbochi au viowevu vingine. Lakini spishi za Zeugloptera bado zina sehemu za kutafuna kama ndugu wao wa oda Trichoptera (Wadudu mabawa-manyoya).

Wachanga wa vipepeo na nondo huitwa viwavi. Hawafanani na wapevu kwa sababu hawana mabawa, wana sehemu za kinywa za kutafuna na wana miguu bandia kwenye fumbatio licha ya miguu sita ya kweli kwenye toraksi. Kwa kawaida viwavi hula majani ya mimea na mara nyingi shina pia na pengine hata matunda. Spishi fulani za viwavi hula wadudu wengine na nyingine ni vidusia.

Mlonge

Mlonge, mlongo, mronge, mrongo, mkimbo au mzunze (Moringa oleifera) ni mti wa jenasi pekee, Moringa, ya familia Moringaceae. Asili ya mti huu ni Uhindi lakini siku hizi hupandwa mahali pengi pa kanda za tropiki na nusutropiki. Hutumika kwa kulisha mifugo, chakula cha watu, kuboresha mashamba, kusafisha maji ya kunywa na mitishamba. Majani yake ni chakula bora (mboga chungu), lakini maganda mabichi, maua, mbegu, mafuta ya mbegu na mizizi hulika pia.

Mti wa mlonge pia umegundulika kuwa ndio mti wenye maajabu zaidi duniani hasa baada ya kufanyiwa utafiti na wanasayansi wa Uingereza. Mti huu una uwezo wa kutibu magonjwa zaidi ya 100 kama vile vidonda vya tumbo, malaria, homa ya matumbo, maambukizo ya mfumo wa mkojo na magonjwa mengine. Mti huu pia umeonekana kuwa na protini nyingi kuliko inayopatikana katika nyama, maziwa, samaki pamoja na maharagwe. Pia mti huu una virutubisho vya Omega-3 ambavyo havipatikani katika maziwa na nyama hivyo kuwa ndio mti wa ajabu zaidi duniani.

Mpapai

Mpapai ni mti wa familia Caricaceae ambao unazaa mapapai.

Mti huo unatoka Meksiko lakini siku hizi hukuzwa kila mahali katika ukanda wa tropiki kwa sababu matunda yake hupendwa sana.

Tafiti mbalimbali zimeonesha kwamba mbegu za papai ni muhimu kwa afya ya binadamu kuliko papai lenyewe; zinaweza kutibu matatizo ya ini, figo, malaria, baadhi ya minyoo na hupunguza unene uliopitiliza.

Mswaki (mti)

Mswaki au msuake ni majina ya miti mbalimbali wa familia Salvadoraceae, lakini spishi kuu iitwayo majina haya ni Salvadora persica. Spishi nyingine ni Dobera glabra na D. loranthifolia zinazoitwa msega na mkupa pia. Miti hii inatokea maeneo makavu ya Afrika na Mashariki ya Kati na hadi Uhindi. Vitawi vya miti hii hutumika kama brashi ya meno na huitwa mswaki pia.

Nondo (mdudu)

Kwa maana nyingine za jina hili tazama nondo (maana)

Nondo ni wadudu wa oda ya Lepidoptera (lepidos = gamba, ptera = mabawa) ambao wanabeba vigamba juu ya mabawa yao. Nondo wanafanana na vipepeo lakini wanatofautiana kwa umbo la vipapasio. Vile vya vipepeo ni kama nyuzi zenye kinundu mwishoni kwao lakini vile vya nondo vina maumbo mbalimbali bila kinundu. Juu ya hiyo takriban nondo wote hukiakia wakati wa usiku na vipepeo hukiakia wakati wa mchana. Kuna zaidi ya spishi 160,000 za nondo.

Sukumawiki

Sukumawiki (pia: sukuma wiki) ni aina ya kabichi isiyoumba 'kichwa' na inayoliwa sana katika Afrika ya Mashariki, hususa nchini Kenya. Inatengenezwa kwa kutumia majani mabichi yanayopikwa. Lakini sukumawiki inaweza kutengenezwa pia kwa kutumia aina nyingine za majani yanayofaa kupikwa.

Jina "sukuma wiki" lamaanisha ya kwamba hii ni njia ya kula kwa siku za wiki bila gharama kubwa hadi kufikia wikendi ambako chakula bora kinapatikana - kama pesa inatosha.

Huliwa mara nyingi pamoja na ugali au chapati. Nyama, samaki au karanga inaweza kuungwa mle.

Wamasai

Wamasai ni kabila la watu wanaopatikana Kenya na Tanzania. Kwa sababu ya mila zao, mavazi tofauti na kuishi karibu na mbuga nyingi za Afrika Mashariki, ni miongoni mwa makabila yanayojulikana zaidi hata nje ya Afrika. Kiasili walikuwa wafugaji na hivyo walihamahama, na sehemu bado wanaishi maisha yale.

Wao wanazungumza Maa, mojawapo ya familia ya lugha za Kinilo-Sahara inayohusiana na Kidinka na Kinuer. Kwa sababu ya uhamiaji, Wamasai ni wazungumzaji wa Kiniloti wa kusini zaidi. Pia wameelimika katika lugha rasmi za Kenya na Tanzania: Kiswahili na Kiingereza.

Utafiti juu ya DNA yao umeonyesha walivyoathiriwa na urithi wa nasaba mbalimbali, hata kutoka nje ya Afrika, lakini hasa wa jamii ya Wakushi wa Afrika Mashariki.

Idadi ya Wamasai ilikadiriwa kuwa 841.622 katika sensa ya 2009 na 800.000 katika Tanzania mwaka 2011 ; kwa jumla inakadiriwa kuwa inakaribia 1.700.000 Makadirio hayo ya Wamasai katika nchi zote mbili huenda ikawa vigumu kuyathibitisha kwa sababu ya umbali wa maeneo ya vijiji vyao vingi, na asili yao ya uhamaji.

Ingawa serikali za Tanzania na Kenya zimeweka mipango kuwahimiza Wamasai kuachana na jadi ya uhamaji, bado wameendelea na desturi hiyo. Hivi majuzi, Oxfam imedai kwamba mtindo wa maisha ya Wamasai lazima ukubaliwe kwa kuzingatia mabadiliko ya hali ya hewa kwa sababu hawana uwezo wa kulima katika majangwa.

Wilaya ya Mufindi

Mufindi ni wilaya iliyopo katika Mkoa wa Iringa nchini Tanzania yenye Postikodi namba 51400. Katika sensa ya mwaka 2002, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 265,829 .

Wilaya imepakana upande wa kaskazini na wilaya za Kilolo na Iringa Mjini, upande wa kusini na mkoa wa Njombe, upande wa mashariki na mkoa wa Morogoro na upande wa magharibi na Mkoa wa Singida.

Mufindi iko sehemu ya Nyanda za Juu za Kusini na sehemu za wilaya ziko mita 2000 juu ya usawa wa bahari. Kwa hiyo kuna baridi na mvua nyingi. Wilayani kuna mashamba makubwa ya chai, misitu ya kupandwa ya Sao Hill inayoongoza kwa kutoa mbao Tanzania na Afrika Mashariki, inastawisha mahindi, maharagwe, viazi, kabichi na pareto.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.