Dola

Dola (kutoka Ar. دولة daulat; nchi, serikali, taifa; ing. state) ni utaratibu wa kisiasa wa jamii katika eneo fulani.

Ufafanuzi wa "Dola"

Fani mbalimbali huwa na maelezo tofauti kiasi juu ya maana ya dola:

 • sheria hufundisha dola kuwa mamlaka ya jamii ya taifa; ina tabia tatu za kimsingi ambazo ni
  • eneo la dola,
  • taifa au watu wa dola na
  • mamlaka ya dola juu ya watu na eneo lake.
 • elimu jamii hufundisha kufuatana na Max Weber dola kuwa jumuiya au jamii ambayo ina mamlaka ya kukubalika ya pekee katika eneo fulani; hivyo ni uhusiano wa utawala wa watu juu ya watu unaofuata haki na sharia.
 • elimu siasa hufundisha dola kuwa muundo wa mamlaka ya umma kwa ajili ya kuratibu mambo ya umma.
 • falsafa hufundisha dola kuwa utekelezaji wa shabaha za kimaadili za kila mtu na jamii kwa pamoja; Hegel alisema dola ni mwendo wa Mungu katika historia; msingi wake ni akili inayotaka kuwa uhalisia.

Aina za Dola

Dola hutokea kwa maumbo mbalimbali kwa mfano jamhuri au ufalme. Dola inaweza kujitegemea kabisa au kuwa sehemu ya shirikisho au muungano kama Muungano wa Madola ya Amerika. Ndani ya maumbo haya kuna njia mbalimbali za kutekeleza mamlaka na kuratibu serikali kwa mfano kwa njia ya demokrasia au udikteta.

Vyombo vya Dola

Kiini cha dola ni utekelezaji wa mamlaka katika eneo fulani. Hapo kuna chombo kinachoitwa serikali chenye mamlaka haya mkononi. Serikali inaangaliwa na taasisi nyingine.

Katika madola ya kisasa kuna mgawanyo wa madaraka wa dola kwa taasisi mbalimbali:

 • bunge huamua juu ya sheria
 • serikali inatekeleza sheria
 • mahakama zinaangalia utekelezaji na kuamua kama kuna mawazo tofauti

VYombo vingine ni matawi mbalimbali ya serikali kulingana na katiba ya dola.

Tazama pia

Angola

Angola ni nchi kubwa iliyopo upande wa kusini magharibi wa bara la Afrika ikipakana na Namibia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Zambia. Upande wa magharibi kuna pwani ndefu ya Bahari Atlantiki. Mkoa wa Kabinda umetenganika na sehemu nyingine za nchi na unapakana na Jamhuri ya Kongo pia.

Angola ni nchi tajiri kwa mafuta na madini: almasi ndiyo muhimu zaidi. Lakini nchi ni maskini kutokana na vita vya miaka 29; kwanza vita vya kupigania uhuru dhidi ya Ureno iliyofuatwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe hadi mwaka 2002.

Nchi yenyewe hasa ni ya kidemokrasia na inajulikana kama Jamhuri ya Angola (kwa Kireno: República de Angola, kwa matamshi ya IPA: /ʁɛ.'pu.βli.kɐ dɨ ɐ̃.'ɣɔ.lɐ/; kwa lugha za wenyeji: Repubilika ya Ngola).

Dola la Roma

Dola la Roma (kwa Kilatini "Imperium Romanum") lilikuwa milki kubwa lililoenea kwa karne kadhaa katika nchi zote zinazopakana na bahari ya Mediteranea (ambayo kwa sababu hiyo iliitwa "Mare Nostrum", yaani "Bahari yetu") na nyinginezo.

Lilianza kwenye mji mkuu wa Roma na rasi ya Italia ikaendelea kuunganisha makabila na mataifa ya nchi nyingi kwenye mabara matatu ya Ulaya, Afrika na Asia.

Kuanzia karne ya 1 KK Watawala wa Dola wakaitwa makaisari: Kaisari wa kwanza alikuwa Augusto.

Nchi nyingi za sasa ziliwahi kuwa sehemu ya Dola la Roma kama vile Uingereza, Ufaransa, Hispania, Italia, Ugiriki na nchi za Balkani upande wa Ulaya, Moroko, Algeria, Tunisia, Libia na Misri upande wa Afrika, na Uturuki, Syria, Lebanon, Palestina, Jordan na hata Irak upande wa Asia.

Idadi ya wakazi imekadiriwa kuwa ilifikia milioni 50-90, yaani asilimia 20 hivi za watu wote duniani wakati huo.

Lugha ya Dola la Roma ilikuwa Kilatini, ila katika sehemu za mashariki pamoja na Kigiriki cha Kale.

Sehemu ya magharibi ya Dola la Roma iliishia mwaka 476 baada ya mapinduzi ya kijeshi dhidi ya Kaisari wa mwisho Romulus Augustulus aliyefukuzwa na jemadari wa Kigermanik wa jeshi la Roma.

Upande wa mashariki Dola la Roma likaendelea hadi mwaka 1453 kwa majina kama "Roma ya Mashariki" au Bizanti.

Dolar ya Marekani

Dolar ya Marekani (pia: dola, US-Dollar, kifupi USD) ni pesa halali ya Marekani. Alama yake ni $.

Dolar ya Marekani inapatikana kwa noti za dola 1, 2, 5, 10, 20, 50 na 100. Kuna pia sarafu ya dola 1.

Dolar moja ina senti 100. Senti huitwa pia "penny" nchini Marekani. Kuna sarafu za nusu dolar (half dollar, senti 50), robo dolar (quarter, senti 25) na sarafu za senti 10 (dime), 5 (nickel) na 1 (penny).

Hadi mwaka 1969 noti ya dolar ya Marekani ilikuwa na ahadi ya kwamba serikali ya Marekani itampatia kila mtu dhahabu kulingana na thamani ya dola hizi akipenda kuzibadilisha.

Usawa huu na thamani ya dhahabu ulifutwa. Leo hii dolar ya Marekani ni pesa ya kuiamini serikali kama pesa zote. Maana yake watumiaji husadiki ya kwamba serikali haitachapisha dola kushinda uwezo wa uchumi na thamani ya bidhaa zilizopo nchini.

Tangu mwisho wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia (1945) dolar ya Marekani imekuwa pesa kuu duniani na sehemu kubwa ya biashara ya kimataifa hukadiriwa kwa dolar hizo. Lakini tangu kupatikana kwa Euro mwaka 1999 umuhimu wa dolar ya Marekani imeanza kupungua polepole. Hata hivyo nchi mbalimbali zimeachana na sarafu zao na kuamua kutumia dolar ya Marekani tu, k.mf. El Salvador.

Jimbo

Jimbo ni eneo fulani lililotengwa kwa ajili ya kurahisisha utawala ndani ya dola au nchi fulani. Neno latumiwa pia kwa vitengo mmndani ya Kanisa.

Kabila

Kabila ni jamii ya binadamu yenye umoja fulani upande wa lugha na utamaduni, si lazima upande wa eneo na utawala wa siasa.

Kwa mfano, katika nchi ya Tanzania kuna makabila zaidi ya 120, kama vile kabila la Wachaga, la Waluguru n.k. Nchini Kenya kuna Wakikuyu, Waribe n.k.

Wengine wanaeleza kwamba makabila yalitokea kabla ya madola na yanaendelea kujitegemea kwa kiasi fulani ndani ya dola.Lakini wengine wanatumia neno hilo kwa upana zaidi.

Kaizari

Kaizari ni cheo cha mfalme mkuu. Neno la Kiswahili limetokana na lugha ya Kijerumani "Kaiser", lakini asili yake ni Kilatini "Caesar".

Karne ya 19

Karne ya 19 ilikuwa kipindi cha miaka mia moja kati ya 1800 na 1900. Kikamilifu kilianza tarehe 1 Januari 1801 na kuishia 31 Desemba 1900.

Kama kila "karne" ni kipindi kinachohesabiwa kwa hiari ya binadamu kwa sababu ni mgawanyo wa kalenda tu - hali halisi, maendeleo na mabadiliko makubwa hayafuati migawanyo ya kalenda ya kibinadamu.

Hata hivyo kipindi hiki cha karne ya 19 kilikuwa kipindi muhimu sana katika historia ya binadamu.

Karne ya 4

Karne ya 4 ilikuwa kipindi cha miaka mia moja kati ya 301 na 400. Kikamilifu kilianza tarehe 1 Januari 301 na kuishia 31 Desemba 400. Namba zake zinafuata hesabu ya miaka "baada ya Kristo".

Kama kila "karne" ni kipindi kinachohesabiwa kwa hiari ya binadamu kwa sababu ni mgawanyo wa kalenda tu: katika hali halisi maendeleo na mabadiliko makubwa hayafuati migawanyo ya kalenda ya kibinadamu.

Kuna mambo mengi yaliyotokea wakati wa karne hii, kama haya yafuatayo.

Kilatini

Kilatini ni lugha ya kihistoria ambayo siku hizi haina tena wasemaji kama lugha ya kwanza, lakini bado hufundishwa katika shule na vyuo na hata kutumiwa kama lugha ya pili. Ilikuwa pia lugha ya kimataifa ya elimu na istilahi nyingi za kisayansi zimetoka katika Kilatini.

Kilatini kilikuwa lugha hai takriban kati ya miaka 500 KK na 600 BK na baadaye lahaja zake mbalimbali ziliendelea na kukomaa kuwa lugha za pekee zinazojulikana kama lugha za Kirumi.

Kilatini ni pia jina la mwandiko au aina ya herufi (alfabeti ya Kilatini) inayotumika kwa lugha nyingi duniani. Hata Kiswahili huandikwa siku hizi kwa herufi za Kilatini kama kwa mfano ukurasa huu wa Wikipedia.

Kilikuwa

lugha ya Dola la Roma (angalia pia Roma ya Kale)

lugha mama ya lahaja zilizoendelea kuwa lugha za Kirumi kama Kiitalia, Kifaransa, Kihispania, Kireno, Kiromania n.k.

lugha ya elimu na sayansi katika Ulaya kwa karne nyingi

lugha rasmi ya serikali katika nchi nyingi za Ulaya kati ya mwisho wa Dola la Roma mwaka 476 BK hadi mnamo 1700 BK

lugha pekee ya liturgia katika Kanisa la Kilatini hadi mwaka 1965Hadi leo ni

lugha ya kidini katika Kanisa Katoliki

lugha rasmi katika nchi ya Vatikano.

Kilatini ina athira kubwa katika lugha ya sayansi na elimu. Hadi leo hufundishwa mashuleni hasa Ulaya.

Kiswahili kimerithi maneno yenye asili ya Kilatini hasa kupitia Kiingereza kilichopokea karibu asilimia hamsini ya maneno yake yote kutoka Kilatini kupitia hasa Kifaransa. Maneno mengine ya Kilatini yameingia Kiswahili kupitia Kireno, Kifaransa n.k.

Kilatini huendelezwa na kukuzwa na wapenzi wa lugha. Kuna misamiati ya "Kilatini cha Kisasa" yenye maneno kwa ajili ya mitambo ya kisasa, mtandao n.k. Wikipedia ya Kilatini ilifikia makala zaidi ya 130,000 kwenye mwaka 2019.

Mali

Kwa maana mengine ya neno hili angalia Mali (maana)

Mali (kwa Kifaransa République du Mali = Jamhuri ya Mali) ni nchi ya Afrika ya Magharibi. Imepakana na Algeria, Mauretania, Niger, Burkina Faso, Cote d'Ivoire na Senegal.

Haina pwani kwenye bahari yoyote.

Sehemu ya juu ni mlima wa Hombori Tondo (mita 1155 juu ya UB) ulioko katikati ya nchi.

Kaskazini sehemu kubwa ya eneo la Mali ni jangwa la Sahara.

Wakazi walio wengi huishi kusini, karibu na mito ya Senegal na Niger.

Mamlaka

Mamlaka (kutoka Kiarabu; kwa Kiingereza "authority" kutoka neno la Kilatini auctoritas) linaweza kutumika kumaanisha haki ya kisheria ya kutumia nguvu ambayo imetolewa na nchi au vyombo vingine vya serikali kama mahakama,bunge na vyombo vya dola.

Neno mamlaka linapotumika katika mashirika au taasisi, huwa linamaanisha chombo kinachotawala ambacho kimepewa nguvu, kwa mfano: Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Morogoro.

Pia neno mamlaka linaweza kumaanisha haki ya kufanya kitu fulani.

Milki ya Osmani

Milki ya Osmani (pia: Ottomani) ilikuwa dola kubwa lililotawala upande wa mashariki wa Mediteranea pamoja na nchi nyingi za Mashariki ya Kati kati ya karne ya 14 na mwaka 1922.

Milki ilianzishwa na Waturuki Waosmani ikachukua nafasi ya ukhalifa wa Waabbasi na Milki ya Bizanti.

Mji wake mkuu ulikuwa Konstantinopoli (leo: Istanbul) na mtawala wake mkuu alikuwa Sultani wa Waosmani. Imani rasmi ya milki ilikuwa Uislamu hata kama katika maeneo mengi idadi kubwa ya wakazi walikuwa Wakristo.

Tabaka la viongozi wa kisiasa na wa kijeshi walikuwa Waosmani waliokuwa Waturuki pamoja na mchanganyiko wa Waislamu kutoka sehemu zote za milki yao, hasa Balkani. Kwenye uwanja wa uchumi na utawala Waosmani walitumia sana Wakristo Wagiriki na Waarmenia kutokana na elimu yao.

Myanmar

Myanmar (pia: Myama; Myamari) ni nchi ya Asia ya Kusini-Mashariki inayojulikana pia kwa jina la Burma au Bama.

Imepakana na China upande wa kaskazini, Laos upande wa mashariki, Uthai kusini-mashariki, Bangladesh na Uhindi magharibi.

Kuna pwani kwenye Bahari Hindi yenye urefu wa km 2,000.

Roma ya Kale

Roma ya Kale ni ustaarabu uliokua kutoka katika mji Roma, ulioanzishwa katika rasi ya Italia kabla ya karne ya 9 KK.

Katika kipindi cha karne kumi na mbili cha uhai wake, ustaarabu wa Roma ulibadilika toka kuwa dola-mji, kwanza ufalme halafu jamhuri ya Roma yenye athira katika Italia, na hadi kuwa milki kubwa. Roma ya Kale ilikuja kutawala Ulaya Magharibi na eneo zima linalozunguka bahari ya Mediteranea kwa njia ya vita au kwa njia ya maungano na maeneo.

Baada ya karne za upanuzi uhamiaji wa mataifa mapya ya Wagermanik pamoja na mashambulio kutoka Asia zilisababisha hatimaye kuanguka kwa Dola la Roma kuanzia karne ya 5 BK.

Sehemu ya magharibi ya milki dola liliporomoka kabisa likiendelea na umoja wa kiutamaduni lililotunzwa hasa na Kanisa Katoliki chini ya uongozi wa Papa wa Roma.

Sehemu ya mashariki ya Dola iliyoongozwa kutoka Konstantinopoli iliendelea. Tabia yake ilibadilika polepole kuwa milki ya Wagiriki ikaitwa baadaye Milki ya Byzanti ikiendelea hadi mwaka 1453, Waturuki walipotwaa mji wa Konstantinopoli na kuimaliza.

Sensa

Sensa ni utaratibu wa kupata na kutunza habari kuhusu idadi ya watu fulanifulani. Pia ni utaratibu wa mara kwa mara na hesabu rasmi ya idadi ya watu hao. Msamiati hutumiwa zaidi kuhusiana na idadi ya kitaifa na sensa ya mlango kwa mlango (kuchukuliwa kila miaka 10 kulingana na mapendekezo ya Umoja wa Mataifa), na ile ya kilimo na biashara.

Msamiati huu umetoholewa kutoka lugha ya Kiingereza (census), lakini una asili ya Kilatini: wakati wa Jamhuri ya Kirumi sensa ilikuwa ni orodha iliyowekwa ili kufuatilia wanaume wenye uwezo wa kufaa kutoa huduma za kijeshi.

Sensa hutofautiana na njia ya sampuli ambapo habari zinapatikana kutoka sehemu ndogo tu ya idadi ya watu, wakati mwingine kama Makisio ya Kisensa. Takwimu za sensa kwa kawaida hutumiwa kwa utafiti, biashara ya masoko, na mipango kama njia bora kwa msingi wa utafiti wa sampuli. Katika baadhi ya nchi, takwimu za sensa hutumiwa kwa kugawanya uwakilishi katika bunge la taifa (wakati mwingine kiutata - tazama mfano Utah v. Evans).

Inatambulika sana kwamba idadi ya watu na makazi ni muhimu kwa ajili ya mipango ya jamii yoyote. Njia za jadi za sensa, hata hivyo, zimekuwa ghali zaidi.

Sheria muhimu kuhusu gharama ya sensa katika nchi zinazoendelea imekuwa dola 1 kwa mtu. Takwimu za msingi zaidi leo ni karibu dola 3. Makadirio haya sharti yachukuliwe kwa uangalifu sana ikizingatiwa kuwa idadi ya shughuli hutofautiana baina ya mataifa mbalimbali yanayojumuishwa (mfano mwanasensa anaweza kukodishwa ama akawa mfanyakazi wa umma).

Gharama katika nchi zilizoendelea ni ya juu zaidi. Gharama kwa sensa ya 2000 nchini Marekani ilikadiriwa kuwa dola bilioni 4.5, zaidi ya dola 15 kwa mtu. Njia mbadala za kupata takwimu zingali zinachunguzwa. Nchi za Skandinavia za Denmark, Finland na Norway zimekuwa zikitumia rejista za kiutawala kwa miaka kadhaa sasa. Sensa nusu na Sampuli zinatumika Ufaransa na Ujerumani.

Serikali

Serikali (kutoka Kiajemi سرکاری, serkari, mamlaka) ni watu na taasisi ndani ya jamii hasa dola vyenye mamlaka ya kutawala na kufanya maazimio kwa wote katika eneo fulani.

Serikali inatunza na kutekeleza sheria, kanuni na miongozo na kuendesha shughuli muhimu za umma.

Shabaha kuu ya serikali ni kutunza amani na usalama wa raia katika jamii.

Ufalme wa Byzanti

Ufalme wa Byzanti (kwa Kigiriki: Βυζαντινή Αυτοκρατορία) ni neno linalotumika kutaja Dola la Roma lilivyoendelea mashariki mwa eneo la kandokando ya bahari ya Mediteranea katika Zama za Kati, ukiwa na makao yake makuu kwenye mji wa Konstantinopoli (ulioitwa pia Bizanti) na kutumia lugha ya Kigiriki.

Katika baadhi ya maana, hasa baada ya kuanguka kwa Dola la Roma Magharibi na mjini Roma penyewe, hujulikana pia kama Dola la Roma Mashariki.

Wabizanti wenyewe walijiona ni bado Dola la Roma likiendelea tu. Watawala walitumia cheo cha "Kaisari" kama awali.

Hata hivyo, kwa wakati mwingi wa historia yake, ulifahamika na wenzao wa Ulaya magharibi kama “Ufalme wa Wagiriki” au “Ufalme wa Konstantinopoli” au "Rhômania".

Lakini majirani wa mashariki kama Waarabu waliendela kuwaita "Waroma" (kwa Kiarabu روم rum).

Bizanti ilipata mapigo mawili makubwa katika historia yake:

Uvamizi wa Waarabu Waislamu kuanzia mwaka 636 uliosababisha kupotea kwa majimbo ya Afrika ya Kaskazini, Misri na Shamu

Uvamizi wa jeshi la Wakristo la Vita vya msalaba walioteka mji wa Konstantinopoli mwaka 1204. Shambulio hili lilisababisha nguvu za ufalme kufifia kabisa. Hata baada ya watawala wa Bizanti kurudi Konstantinopoli walikosa nguvu ya kujihami dhidi ya Waturuki Waosmani. Hatimaye hao waliteka Konstantinopoli mwaka 1453 na kumaliza kabisa Bizanti uliokuwa umetunza urithi wa Roma ya Kale hadi wakati ule.

Ujerumani

Ujerumani (pia: Udachi, kwa Kijerumani: Deutschland) ni nchi ya Ulaya ya Kati.

Imepakana na Denmark, Poland, Ucheki, Austria, Uswisi, Ufaransa, Luxemburg, Ubelgiji na Uholanzi.

Ni nchi yenye watu wengi katika Ulaya, isipokuwa Urusi ina watu zaidi.

Uchumi wa Ujerumani una uwezo mkubwa: ni nchi inayouza bidhaa nyingi nje kushinda mataifa yote ya dunia.

Muundo wake kiutawala ni shirikisho la jamhuri lenye majimbo 16 ndani yake na kila jimbo lina kiwango cha kujitawala.

Wilaya

Wilaya ni mgawanyo wa kiutawala au eneo lililotengwa kwa ajili ya utawala. Mikoa ya Tanzania na Kenya imegawiwa kwa wilaya.

Asili ya neno ni Kiarabu "ولاية" (wilaayatun - Kituruki: vilayet). Katika Dola la Osmani "vilayet" ilikuwa ngazi ya kwanza ya mgawanyo wa kiutawala ikimaanisha jimbo au mkoa. Mkuu wake au gavana alikuwa na cheo cha "Wali". Neno hili la "wilaya" limepatikana katika nchi nyingi zilizoathiriwa na utamaduni wa Uislamu au lugha ya Kiarabu kama vile Uturuki, Algeria, Tunisia, Oman, Mauritania, Sudan, Malaysia, Indonesia, Afghanistan, Tajikistan, Turkmenistan na Uzbekistan.

Katika Kiarabu cha Kisasa "wilaayatun" inamaanisha pia dola ndani ya shirikisho - kwa mfano madola kama vile Texas ndani ya Marekani.

Katika matumizi ya Kiswahili huko Kenya na Tanzania "wilaya" imekuwa mgawanyo wa ngazi ya pili yaani ni kitengo chini ya ngazi ya kwanza ya mikoa. Vitengo vya wilaya ni tarafa. Na vitengo vya tarafa ni kata zinazoitwa shehia katika Zanzibar na chini yake vijiji au mitaa.

Algeria ni nchi nyingine ambako wilaya inamaanisha ngazi ya pili ya kiutawala.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.