Dayosisi

Dayosisi (kwa Kilatini dioecesis, kutokana na Kigiriki διοίκησις, dioikesis, yaani "utawala") ni jina linalotumika katika madhehebu mbalimbali ya Ukristo (kwa mfano Walutheri na Waanglikana kumaanisha kitengo kilichopo chini ya usimamizi wa askofu katika eneo fulani.

Wakatoliki wanaoongea Kiswahili wanaiita jimbo, lakini kwa lugha nyingine wanatumia neno kama hilo bila ya kulitafsiri; kwa mfano "diocese" (Kiingereza), "diocesi" (Kiitalia) au "diocèse" (Kifaransa).

Historia

Mwanzoni "dayosisi" ilikuwa kitengo cha utawala wa serikali katika Dola la Roma; dayosisi moja ilijumlisha majimbo kadhaa. Baada ya uenezaji wa Ukristo katika Dola la Roma Kanisa lilianza kutumia mipaka ya utawala wa serikali kwa ajili ya vitengo vyake na kwa njia hiyo muundo wa dayosisi ulikuwa pia muundo wa utawala ndani ya Kanisa. Baada ya kuporomoka kwa Dola la Roma jina hilo halikutumiwa tena upande wa serikali lakini likaendelea ndani ya Kanisa kwa ajili ya eneo lililo chini ya askofu.

Katika Kanisa Katoliki

Mtaguso wa pili wa Vatikano uliweka mbele waamini kuliko eneo, hivi kwamba yanaweza kuwepo majimbo yasiyo na eneo maalumu, hasa kutokana na wingi wa uhamiaji uliopo siku hizi: "Jimbo ni sehemu ya Taifa la Mungu iliyokabidhiwa kichungaji kwa Askofu, akisaidiwa na mapadri wake, hivi kwamba kwa kuambatana na Mchungaji wake, na kuungana ndani ya Roho Mtakatifu kwa njia ya Injili na ya Ekaristi takatifu, iunde Kanisa maalumu, ambamo linakuwemo na kutenda Kanisa la Yesu Kristo, lililo Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume" (Christus Dominus) 11.

Kwa kawaida majimbo ya jirani yanaunda kanda ya Kanisa ("metropolitani"), mojawapo likiwa jimbo kuu (askofu wake ni askofu mkuu na anaitwa "metropoliti"). Majimbo yaliyo chini yake yanaitwa "sufragani".

Viungo vya nje

Christianity Symbol.png Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Dayosisi kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.
Askofu

Askofu ni mtu mwenye cheo cha juu katika Kanisa. Kwa kawaida huliongoza katika eneo la jimbo dayosisi akisimamia shirika au parokia nyingi.

Askofu mkuu

Askofu mkuu ni cheo cha askofu kiongozi anayesimamia maaskofu katika jimbo la kanisa lenye dayosisi mbalimbali.

Asili ya neno lenyewe ni Kigiriki αρχή arché (mwanzo, wa kwanza). Sehemu ya pili ni neno la Kigiriki επίσκοπος episkopos (mwangalizi) lililofikia Kiswahili kupitia umbo la Kiarabu uskuf.

Bulongwa

Bulongwa ni makao makuu ya Wilaya ya Makete katika Mkoa wa Iringa, Tanzania. Wakati wa wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 3,824 walioishi humo. Msimbo wa posta ni 59514

Bulongwa iko kwenye sehemu ya magharibi ya milima ya Livingstone kwenye kimo cha mita 2100 juu ya UB. Hakuna joto kali na wakati wa Juni - Agosti jalidi hutokea. Mvua unatoeka kati ya Novemba hadi Mei.

Mji ni kitovu cha dayosisi ya kusini ya Kanisa la Kiluteri Tanzania Kati, kuna hospitali ya kanisa na ofisi ya dayosisi.

Bumbuli

Bumbuli ni jina la kata ya Wilaya ya Lushoto katika Mkoa wa Tanga, Tanzania. Kwa mujibu wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ina wakazi wapatao 10,159 waishio humo.

Wenyeji wa Bumbuli ni Wasambaa.

Bumbuli imezungukwa na milima kila upande, mji wenyewe wa Bumbuli upo chini ya mlima mkubwa unaoitwa Maduda ambao ni mshikano wa mwamba mkubwa ulioanzia sehemu inayoitwa Kungutana na kuendelea mpaka eneo la Mmanyai ambapo mwamba huo unaishia.

Kwa upande wa kaskazini mashariki upo mlima mkubwa unaoitwa Kizimba. Mlima huu huaminika sana kwa kuonyesha dalili za mvua kubwa mara wingu linapotanda juu yake.

Kutokana na hali nzuri ya hewa ya eneo hili, wamisionari Wajerumani wa kwanza kufika milima ya Usambara walivutiwa sana na eneo hili na kujenga hospitali kubwa ambayo kwa sasa inamilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini Mashariki.

Hai Mjini

Hai Mjini ni makao makuu ya Wilaya ya Hai katika Mkoa wa Kilimanjaro, Tanzania. Wakati wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 34,980 walioishi humo. Msimbo wa posta ni 25312.

Mji wa Hai ulikua kutoka kwa kijiji cha Bomang'ombe kilichopo kwenye barabara kuu kutoka Arusha kwenda Moshi Mjini.

Hapo iko Chuo cha Ufundi wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini kinachotoa mafunzo ya useremala, ufundi metali, ushonaji na upishi. Ni mahali pekee Tanzania ambako vinanda filimbi vinatengenezwa.

Jimbo

Jimbo ni eneo fulani lililotengwa kwa ajili ya kurahisisha utawala ndani ya dola au nchi fulani. Neno latumiwa pia kwa vitengo mmndani ya Kanisa.

Kahama (mji)

Kahama ni mji ulio makao makuu ya wilaya ya Kahama katika Mkoa wa Shinyanga wenye halmashauri yake ya pekee hivyo mwenye hadhi ya wilaya. Halmashauri ilianzishwa baada ya kugawa kwa Wilaya ya Kahama ya awali. Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 242,208. Mji huu ni maarufu kwa uchimbaji wa dhahabu. Pia ni mji wa pili kwa mapato kati ya halmashauri za wilaya, ikitanguliwa na Kinondoni na kufuatiwa na Mufindi.

Tangu 1984 mji umekuwa makao makuu ya dayosisi ya Kahama ya Kanisa Katoliki.

Kanisa kuu

Kanisa kuu ni jina la heshima la jengo la ibada la madhehebu mbalimbali ya Ukristo ambalo Askofu wa jimbo (dayosisi) fulani analitumia kwa kawaida kutekeleza kazi yake kama mchungaji mkuu wa waamini wake, kama vile kuhubiri na kufundisha Neno la Mungu, kutakasa watu kwa sakramenti na sala mbalimbali na kuwaunganisha wote katika kumfuata Yesu pamoja.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) ni muungano wa Kilutheri katika nchi ya Tanzania.

Mwaka 1938 makanisa saba ya Kilutheri yaliungana kama Muungano wa Makanisa ya Kilutheri, na tarehe 19 Juni 1963 yalikuwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.Lengo la KKKT ni kuwapa watu nafasi ya kumfahamu Yesu Kristo ili kupata uzima wa milele. Kanisa limejengwa juu ya msingi wa Yesu Kristo, linaongozwa na Neno la Mungu kama linavyopatikana katika Agano la Kale na Agano Jipya (Biblia ya Kikristo), na limeimarishwa katika sakramenti.

KKKT linaongozwa na Mkuu wa kanisa (Askofu Mkuu) na maaskofu ishirini na nne kutoka dayosisi ishirini na nne, wakiwa na wanachama zaidi ya milioni 6,3 wanaolifanya kuwa la pili duniani kati ya makanisa ya Kilutheri (baada ya lile la Uswidi).

Ofisi kuu ya KKKT iko katika mji wa Arusha.

KKKT lina uhusiano na All Africa Conference of Churches (AACC), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Lutheran World Federation (LWF) na Lutheran Mission Cooperation (LMC).

KKKT ni chama kinachowapa wanachama chake nafasi ya kumwabudu Mungu, kupata elimu ya Kikristo na huduma nyingi nyingine.

Kasulu

Kasulu ni mji wa Mkoa wa Kigoma magharibi mwa Tanzania yenye msimbo wa posta 47301. Inatawaliwa na halmashauri yake, hivyo huwa na hadhi ya wilaya tangu enzi za ukoloni.

Wakati wa sensa ya mwaka 2012 ilikuwa na wakazi 208.244. Eneo la manispaa ni km² 911.Awali mji wa Kasulu ulitawaliwa pamoja na wilaya ya Kasulu Vijijini kama wilaya moja ila tangu 2012 ni wilaya mbili za pekee.

Kasulu iko karibu na mpaka wa Burundi. Baada ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi wakimbizi wengi walikimbia Tanzania na makambi makubwa yalijengwa karibu na mji wa Kasulu. Makambi haya ni Muyovosi, Mtabila I and Mtabila II. Mnamo mwaka 2000 idadi ya wakimbizi ilifikia 90,000.

Makambi yaliongeza biashara ya eneo lakini yalileta pia matatatizo kama kupanda kwa bei na upungufu wa usalama kwa sababu ujambazi ulizidi.

Kasulu ni makao makuu ya Dayosisi ya Magharibi ya Kanisa Anglikana Tanzania. Askofu wake alikuwa ni Gerard Mpango. Kanisa kuu ni St Andrew's Cathedral.

Taasisi muhimu ni chuo cha ualimu cha Kasulu Teacher Training College.

Kasulu kuna shule mbalimbali pamoja Kasulu Bible College ya Kanisa la Kianglikana.

Korogwe (mji)

Korogwe ni mji upande wa Kaskazini-Mashariki wa Tanzania ambao ni makao makuu ya Wilaya ya Korogwe. Tangu kupata halmashaur yake ni moja kati ya wilaya 10 za Mkoa wa Tanga kwenye pwani ya Tanzania.

Mwaka 2012 mji ulikuwa na wakazi 68,308 walioishi katika kata 8 za eneo lake.

Mwaka 2012 eneo la mji wa Korogwe lilitengwa na Wilaya ya Korogwe ya awali na kuwa na halmashauri yake ya pekee.

Pia ni makao makuu ya Dayosisi ya Kanisa la Anglikana ya Tanga.

Matamba

Matamba ni jina la kata ya Wilaya ya Makete katika Mkoa wa Njombe, Tanzania. Wakati wa wa sensa iliyofanyika mwaka wa 2012, kata ilikuwa na wakazi wapatao 10,441 walioishi humo. Msimbo wa posta ni 59510

Matamba ni makao makuu ya dayosisi ya kusini magharibi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania.

Mpanda (mji)

Mpanda ni makao makuu na pia mji mkubwa wa Mkoa wa Katavi katika magharibi ya Tanzania. Ni kitovu muhimu cha biashara ya mazao kama mahindi na mpunga kuna pia dalili ya uchumi wa madini hasa dhahabu katika mazingira yake.

Mji umekua sana kuanzia wakazi 46,000 mwaka 2002 hadi kufikia idadi ya wakazi 102,000 wakati wa sensa ya 2012. Hadi mwaka 2014 hapakuwa na barabara za lami bali njia za udongo pekee hivyo usafiri huwa na shida wakati wa mvua. Kuna njia ya reli kutoka hapa hadi Kaliua inapoungana na Reli ya Kati. Safari ya reli hadi Tabora inachukua masaa 10 - 12. Mabasi yanaenda kila siku Sumbawanga (masaa 5), Mbeya na Tabora (masaa 9). Tangu kuwa makao makuu ya mkoa wa Katavi uwanja wa ndege uliboreshwa mwaka 2012.

Upande wa dini kuna makao makuu ya dayosisi wa Kikatoliki pamoja na dayosisi ya Anglika ya Ziwa Rukwa na makanisa ya Moravian, AIC, Assemblies na pia msikiti mbalimbali.

Papa Silvester III

Papa Silvester III alikuwa papa kuanzia Januari hadi Mei 1045 baada ya Papa Benedikto IX kufukuzwa upapani mnamo Septemba 1044. Jina lake la kuzaliwa lilikuwa Yohane Crescenzi.

Alilazimishwa kujiuzulu akafuatwa na Papa Benedikto IX aliyekuwa mtangulizi wake.

Alirudi katika dayosisi yake na kufariki mwaka 1063.

Parokia

Parokia ni muundo mmojawapo wa zamani sana wa Kanisa Katoliki, ambao umuhimu wake unatokana na kwamba ni sehemu ya jimbo (dayosisi) unapofanyika uchungaji wa kila siku chini ya kasisi anayemwakilisha Askofu.

Kiini cha maisha ya parokia ni adhimisho la Ekaristi siku ya Jumapili, ambapo jumuia nzima ya Kikristo ya eneo husika inakusanyika isikilize Neno la Mungu, imsifu Mungu na Kumega mkate.

Sinodi

Sinodi (kwa Kiingereza "synod", kutoka maneno ya Kigiriki σύν, syun, "pamoja" na όδος, odos, "njia" = syunodos, yaani kufuata "njia ya pamoja", kwa hiyo "mkusanyiko" au "mkutano") ni mkutano wa Kanisa la Kikristo ambao huunganisha wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za Kanisa au eneo maalumu ndani ya Kanisa kama sinodi.

Kiasili sinodi ilikuwa mkutano wa maaskofu wa eneo fulani.

Wakati mwingine neno "mtaguso" hutumiwa kwa kutaja sinodi ya maaskofu wote, kwa mfano mtaguso mkuu ni mkutano wa maaskofu wote wa Kanisa Katoliki duniani.

Mara nyingi mkutano mkuu wa dayosisi au wa jimbo la Kanisa huitwa pia "sinodi".

Katika madhehebu ya Kiprotestanti sinodi hujumlisha wachungaji pamoja na walei.

Wapresbiteri hutumia neno "sinodi" kwa ajili ya mikoa yao ikitawaliwa na sinodi, yaani mkutano wa wajumbe kutoka shirika mbalimbali.

Vikarieti ya Kitume

Vikarieti ya Kitume ni aina mojawapo ya majimbo ya Kanisa Katoliki ambayo haijafanywa dayosisi kamili, ingawa mara nyingi inaongozwa na askofu: ni kwa sababu huyo anaongoza kwa niaba ya Papa, hasa katika eneo la umisionari. Ndiyo maana anaitwa kwa Kilatini "Vicarius Apostolicus" (yaani "Makamu wa Kitume", ambapo jina hilo la mwisho linadokeza mamlaka ya Papa kama mwandamizi wa Mtume Petro).

Waanglikana

Waanglikana ni Wakristo wa madhehebu yenye asili ya Uingereza.

Katika karne ya 16 mfalme Henry VIII alitenga Kanisa la nchi hiyo na Kanisa Katoliki.

Baada ya farakano hilo, yalifanyika mabadiliko mbalimbali upande wa imani, ibada na sheria kuelekea Uprotestanti. Hata hivyo mwelekeo wa Kikatoliki uliendelea kuwepo, na bado una nguvu, hasa katika baadhi ya dayosisi. Hasa miaka hii ya mwisho mvutano kati ya pande hizo mbili umeongezeka hata kusababisha umoja kulegea.

Katika karne zilizofuata, kutokana na uenezi wa himaya ya Uingereza duniani, Anglikana ilienea sehemu nchi, na leo ina wafuasi wengi hasa Afrika (Nigeria, Uganda n.k.). Kwa jumla wanazidi milioni 80.

Majimbo yake 38 yanajitegemea, lakini yanaunda ushirika mmoja. Maaskofu wake wote wanakutana Lambeth kila baada ya miaka 10 chini ya Askofu mkuu wa Canterbury.

Wilaya ya Mbinga

Wilaya ya Mbinga ni wilaya moja ya Mkoa wa Ruvuma yenye postikodi namba 57400 .. Katika sensa ya mwaka 2012, idadi ya wakazi wa wilaya hiyo ilihesabiwa kuwa 353,683 .

Wilaya hii imepakana na mkoa wa Iringa upande wa kaskazini, wilaya za Songea mjini na Songea vijijini upande wa mashariki, Msumbiji upande wa kusini na Ziwa Nyassa upande wa magharibi.

Sehemu kubwa ya eneo lake iko ndani ya milima inayoongozana na pwani la ziwa pamoja na mwambao wa ziwa. Wilaya imeona maendeleo kadhaa kutokana na barabara mpya na kilimo cha kahawa inayostawi vizuri katika hali ya hewa mlimani. Mwaka 2012 maeneo ya wilaya ya Mbingwa yalitengwa kuwa wilaya ya Nyasa.

Mji wa Mbinga ni makao makuu ya dayosisi ya Kikatoliki.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.