Bahari ya Mediteranea

Bahari ya Mediteranea (pia: Bahari ya Kati) ni bahari ya pembeni ya Atlantiki kati ya mabara ya Afrika, Ulaya na Asia ya Magharibi. Eneo lake ni takriban milioni 2,5 km². Kina chake kirefu ni 5,267 m. Ina kanda ya hali ya hewa ya pekee pamoja na mimea na wanyama.

Neno "Mediteranea" limetokana na lugha ya Kilatini likiunganisha maneno ya "medium" (inamaanisha "kati ya, katikati") na "terra" (inamaanisha "bara"). Kwa hiyo neno lenyewe linamaanisha "Bahari katikati ya bara".

Katika lugha ya Biblia Kiebrania iliitwa "Bahari ya Magharibi" au "Bahari Kuu"; Waroma wa Kale waliotwala nchi zote zinazopakana na Bahari ya Mediteranea waliita "mare nostrum" yaani "bahari yetu". Waarabu na Waturuki wanaiita "Bahari Nyeupe" (kwa Kituruki: Akdeniz; kwa Kiarabu: البحر الأبيض al-baHr-al-abyaD)

Mediterranean Sea 16.61811E 38.99124N
Bahari ya Mediteranea jinsi inavyoonekana kutoka chombo cha angani
Mediterranean Relief
Ramani ya Bahari ya Mediteranea

Jiografia

Bahari ya Mediteranea ni bahari, si ziwa, kwa sababu imeunganishwa na Atlantiki kwa njia ya mlango wa bahari wa Gibraltar.

Ina bahari za pembeni zake ambazo ni pamoja na Bahari Nyeusi, Bahari ya Aegean, Bahari ya Tyrrheni na mengine. Bahari Nyeusi inaunganishwa kwa njia ya mlangobahari wa Dardaneli, Bahari ya Marmara na mlangobahari wa Bosporus.

Tangu mwaka 1869 kuna pia njia ya maji kati ya Mediteranea na Bahari ya Shamu ambayo ni Mfereji wa Suez.

Kuna visiwa vingi sana hasa kati ya Ugiriki na Uturuki. Visiwa vikubwa ni Korsika, Sardinia, Sisilia, Kreta, Rhodos na Kibros.

Nchi zinazopakana

Leo hii kuna nchi au madola 22 zinazopakana na Bahari ya Mediteraneo:

Misri, Libya, Tunisia, Algeria na Moroko
Uturuki, Syria, Lebanon, Israel, Palestina (Gaza) na Misri
Hispania, Ufaransa, Monako, Italia, Malta (funguvisiwa), Slovenia, Kroatia, Bosnia - Herzegovina, Montenegro, Albania, Ugiriki, Uturuki, Kibros (Cyprus, kisiwa).
Albania

Jamhuri ya Albania ni nchi ya Ulaya Kusini Mashariki. Imepakana na Montenegro, Kosovo, Masedonia Kaskazini na Ugiriki. Upande wa magharibi kuna pwani ya ghuba ya Adria ya bahari ya Mediteranea.

Albania ni kati ya nchi zinazoendelea na imeomba kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Mji mkuu ni Tirana (wakazi 418,495).

Aleksandria

Aleksandria (pia: Alexandria au Iskandiria; kwa Kigiriki Ἀλεξάνδρεια, Alexandreia; kwa Kiarabu: الإسكندرية, al-iskandariya) ni mji mkubwa wa pili wa Misri na bandari muhimu kwenye Bahari ya Mediteranea.

Uko kando ya delta ya Nile kaskazini mwa Misri takriban 225 km kutoka Kairo.

Algeria

Algeria (pia: Aljeria ; kwa Kiarabu: الجزائر al-Jazā’ir; kwa Kiberber: Dzayer, ⴷⵣⴰⵢⴻⵔ) au kwa jina rasmi "Jamhuri ya kidemokrasia ya watu wa Algeria" ni nchi ya Afrika ya Kaskazini-Magharibi. Imepakana na bahari ya Mediteranea, Moroko, Sahara ya Magharibi, Mauretania, Mali, Niger, Libya na Tunisia.

Algeria ni nchi kubwa kuliko zote za Afrika lakini sehemu kubwa ya eneo lake iko katika jangwa la Sahara.

Jina la nchi limetokana na mji mkuu unaoitwa kwa jina lilelile "al-jaza-ir" kama nchi ya leo kwa lugha ya Kiarabu.

Gibraltar

Gibraltar ni eneo la ng'ambo la Uingereza ambalo linaundwa na rasi ndogo katika bahari ya Mediteranea kwenye ncha ya kusini ya rasi ya Iberia katika Ulaya ya Kusini. Imepakana na Hispania.

Hispania

Hispania (kwa lugha ya wenyewe: España, kwa Kiingereza Spain) ni nchi ya Ulaya ya kusini-magharibi. Imepakana na Ufaransa, Andorra, Ureno na eneo la Kiingereza la Gibraltar.

Kuna pwani ndefu ya Bahari ya Mediteranea na pia ya Atlantiki.

Hispania bara ni sehemu kubwa ya rasi ya Iberia. Visiwa vya Baleari kwenye Mediteranea na Visiwa vya Kanari katika Atlantiki pamoja na miji ya Afrika ya Kaskazini Ceuta na Melilla ni sehemu za Hispania.

Mji mkuu ni Madrid ambayo ni pia mji mkubwa wa nchi.

Eneo la nchi ni km² 500,000 nalo lina wakazi 46.733.038 (2018).

Mfalme Felipe VI amevaa taji mwaka 2014, akishika nafasi ya baba yake Juan Carlos I, anayeheshimiwa sana kwa sababu aliongoza taifa katika mabadiliko ya kutoka udikteta wa jenerali Francisco Franco kuelekea demokrasia. Hasa tendo la mfalme la kuzuia mapinduzi wa kijeshi linakumbukwa sana.

Muundo wa serikali ni Ufalme wa Kikatiba, hivyo kisheria madaraka ya mfalme ni madogo.

Utawala umo mikononi mwa serikali inayochaguliwa na bunge linaloitwa "Las Cortes likichaguliwa kwa kura za kidemokrasia.

Kigiriki

Kigiriki (pia: Kiyunani) ni lugha ya Kihindi-Kiulaya inayotumiwa hasa nchini Ugiriki. Maandishi yake yamejulikana tangu miaka 3500 iliyopita. Hakuna lugha nyingine duniani inayozungumzwa hadi leo yenye historia ndefu kuliko hii, isipokuwa Kichina.

Kigiriki ni muhimu sana kwa utamaduni wa kisasa kwa sababu ya kutoa michango mingi kwa lugha ya sayansi, teknolojia na utamaduni. Fikra nyingi muhimu zilionekana mara ya kwanza kwa Kigiriki na falsafa iliyojadiliwa na kuandikwa kwa lugha hii. Istilahi nyingi za kisayansi zimetoka katika Kigiriki.

Alfabeti ya Kigiriki ilikuwa msingi wa alfabeti nyingine mbili, za Kilatini na Kikirili, pia kwa miandiko ya abijadi kama herufi za Kiarabu au za Kiebrania. Kiswahili huandikwa leo kwa herufi za Kilatini.

Kati ya maandiko muhimu ya Kigiriki ni yale ya wanafalsafa kama Plato na Aristoteles na pia baadhi ya maandiko ya Biblia ya Kikristo (Agano Jipya pamoja na Deuterokanoni), mbali ya tafsiri ya kwanza ya Biblia ya Kiebrania maarufu kwa jina la Septuaginta (karne ya 2 KK).

Kati ya karne ya 3 KK hadi karne ya 6 BK Kigiriki kilikuwa lugha ya kimataifa katika eneo kubwa la kandokando ya bahari ya Mediteranea pamoja na Mashariki ya Kati.

Lugha imeendelea kubadilika kisarufi, kimatamshi na pia kimsamiati. Hivyo Kigiriki cha kale kimekwisha, hakizungumzwi tena na watu, lakini bado kinafundishwa katika shule na vyuo vingi, hasa Ulaya.

Leo hii katika nchi ya Ugiriki kuna lugha ya Kigiriki Kipya kinachoendela kuandikwa kwa herufi zilezile.

Lebanoni

Lebanoni (kwa Kiarabu: لبنان ) ni nchi ndogo ya Mashariki ya Kati katika Asia ya Magharibi kando ya Bahari ya Mediteranea.

Imepakana na Syria na Israel.

Mkoa wa Antalya

Mkoa wa Antalya ni moja kati mikoa 81 ya Uturuki. Mkoa upo mjini kusini-mashariki mwa pwani ya Mediteranea, kati ya Milima ya Taurus na Bahari ya Mediteranea. Mji mkuu wake ni Antalya wenye idadi ya wakazi takriban 714,000.

Mkoa wa Mersin

Mersin ni jina la mkoa uliopo mjini kusini mwa nchi ya Uturuki. Mkoa upo kwenye pwani ya Bahari ya Mediteranea kati ya Antalya na Adana. Mji mkuu wake ni Mersin.

Mto

Mto ni mwendo asilia wa maji yanayofuata njia yake kwenye mtelemko hadi mdomoni wake.

Nile

Mto Nile (pia: Naili; kwa Kiarabu: ‏ ,النيل‎ an-nīl) ni mto mkubwa upande wa mashariki ya bara la Afrika. Mara nyingi hutajwa kuwa pia ni mto mrefu kabisa duniani kushinda mto Amazonas. Kutoka Ziwa la Viktoria Nyanza hadi mdomo wake kwenye Bahari ya Mediteranea Nile inavuka nchi za Uganda, Sudan Kusini, Sudan na Misri kwa urefu wa km 6,650.

Beseni la Nile hukusanya maji ya eneo linalojumlisha 10% za eneo la Afrika yote au km² 3,349,000. Takriban watu milioni 250 hukalia beseni hilo.

Roma

Roma (pia: Rumi) ndio mji mkuu ("Roma Capitale") wa Jamhuri ya Italia.

Uko katika makutano ya mito ya Tiber na Aniene karibu na Bahari ya Mediteranea.

Roma una wakazi milioni 2,870,336 katika eneo la km² 1,287.36.

Ndani ya mji wa Roma lipo eneo la mji wa Vatikano ambao ni nchi ya kujitawala chini ya Papa wa Kanisa Katoliki.

Sisilia

Sisilia (kwa Kiitalia Sicilia) ni kisiwa kikubwa cha Italia na cha bahari ya Mediteranea yote, ikiwa na eneo la kilomita mraba 25711.

Iko kusini kwa rasi ya Italia, ng'ambo ya mlangobahari wa Messina.

Sisilia pamoja na visiwa vidogo vya jirani ni pia mkoa wa nchi wenye katiba ya pekee.

Idadi ya wakazi ni watu 5,077,487 (2015), ambao kati yao 98% ni raia wa Italia.

Mji mkuu ni Palermo (wakazi 677,854).

Slovenia

Slovenia ni nchi ya Ulaya ya Kati, mashariki kwa milima ya Alpi.

Imepakana na Italia, ghuba ya Adria ya bahari ya Mediteranea, Kroatia, Hungaria na Austria.

Mji mkuu pia mji mkubwa ni Lyublyana (kwa Kislovenia: Ljubljana).

Ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na wa Umoja wa Ulaya.

Syria

Syria au Siria (kwa Kiarabu: سوريا au سورية ) ni nchi ya Mashariki ya Kati au Asia ya Magharibi.

Imepakana na Lebanon, Israel, Yordani, Iraq na Uturuki.

Kuna pwani kwenye bahari ya Mediteranea.

Nchi inatajwa pia kwa jina la "Shamu" katika maandiko ya Kiswahili, ingawa neno hili lamaanisha zaidi eneo la kihistoria ambalo lilikuwa kubwa kuliko Syria ya leo.

Tunisia

Tunisia (kirefu Jamhuri ya Tunisia - kwa Kiarabu الجمهرية التونسية, al-Jumhūrīya at-Tūnisīya) ni nchi ya Afrika ya Kaskazini inayopakana na Bahari ya Mediteranea, Libya na Algeria.

Mji mkuu ni Tunis (wakazi 728 453) ulioko mahali pa Karthago ya kale.

Ugiriki

Ugiriki (pia: Uyunani; kwa Kigiriki: Ελλάδα, Ellada, au Ελλάς, Ellas) ni nchi ya Ulaya Kusini-Mashariki katika kusini ya rasi ya Balkani.

Imepakana na Albania, Masedonia Kaskazini, Bulgaria na Uturuki.

Upande wa kusini-magharibi na kusini-mashariki kuna pwani ndefu kwenye Bahari ya Mediteranea.

Baharini huko kuna visiwa vingi sana ambavyo ni sehemu za Ugiriki.

Ugiriki ni nchi yenye historia ndefu na maarufu sana, hata inaitwa "nchi mama ya Ulaya".

Lugha ya Kigiriki inaendelea kuandikwa kwa Alfabeti ya Kigiriki inaotumiwa tangu miaka 3000 iliyopita, lakini lugha yenyewe imebadilika. Wagiriki wa leo hawaelewi tena Kigiriki cha Kale moja kwa moja.

Wakazi wengi wanafuata dini ya Ukristo, hasa katika Kanisa la Kiorthodoksi la Kigiriki (97%). 1.3% ni Waislamu.

Ugiriki ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya tangu 1981.

Ulaya

Ulaya (asili ya jina ni neno la Kiarabu ولاية, wilaayatun; inaitwa pia Uropa) ni bara lenye eneo la km² 10,600,000 tu, lakini wakazi ni milioni 700.

Wengi wenye asili ya Ulaya wakati wa ukoloni walitawanyika duniani, hasa Amerika, wakiathiri kote upande wa lugha, utamaduni na dini.

Ziwa Viktoria

Ziwa Viktoria (pia: Ziwa Nyanza au Ziwa Ukerewe) ni ziwa kubwa la Afrika ya Mashariki lililopo baina ya Tanzania, Kenya na Uganda. Eneo la maji ya ziwa limegawanywa 49% (km2 33,700) nchini Tanzania, 45% (km2 31,000) nchini Uganda, na 6% (km2 4,100) nchini Kenya.

Ziwa Viktoria lipo mita 1134 juu ya usawa wa bahari na lina eneo la kilometa za mraba zaidi ya 68,100. Hivyo ni ziwa kubwa kuliko yote barani Afrika, na la pili duniani, baada ya Ziwa Superior ambalo lipo Amerika ya Kaskazini.

Ziwa hili linapata maji yake mengi kutokana na mvua (80%) na kutoka vijito vingi vidogo. Mto mkubwa unaoingia Viktoria ni Mto Kagera unaotiririka kutoka magharibi.

Maji ya ziwa Viktoria yanatoka na kumiminika kwenye mto Nile na kuelekea bahari ya Mediteranea kwa umbali wa maili 4,000.

Ziwa hilo lina kina cha wastani cha mita 40 na mwambao wa urefu wa kilomita 4,828, visiwa vyake vikiwa vimechangia 3.7% ya urefu huu.

Ziwa hilo liliwahi kukauka kabisa mara kadhaa tangu lilipoanza miaka 400,000 iliyopita.

Lugha zingine

This page is based on a Wikipedia article written by authors (here).
Text is available under the CC BY-SA 3.0 license; additional terms may apply.
Images, videos and audio are available under their respective licenses.